VIDEO: Mahakama yasogeza mbele hukumu ya mgogoro wa CUF

Muktasari:

  • Leo Ijumaa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga Machi 17, 2019 kutoa hukumu ya kesi ya mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeshindwa kutoa hukumu ya mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) na badala yake imeisogeza mbele hadi Machi 17, 2019.

Hukumu hiyo ilitarajiwa kutolewa leo Ijumaa, Februari 22, 2019 na Jaji Benhajj Masoud aliyekuwa akiisikiliza kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini  wa chama hicho. Hukumu hiyo imeahirishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Sharmillah Sarwatt.

Akiahirisha hukumu hiyo Naibu Msajili, Sarwatt amesema Jaji Masoud ambaye alitarajiwa kuisoma anakabiliwa na majukumu mengine.

“Hivyo nina ahirisha usomaji wa hukumu hii hadi Machi 17 mwaka huu,” amesema Naibu Msajili Sarwatt akitaja tarehe hiyo baada ya kuwasilishwa na karani wa Jaji Masoud.

Hata hivyo, tarehe hiyo itakuwa ni siku ya Jumapili siku ambayo huwa hakuna shughuli za kimahakama.

Profesa Lipumba ambaye Agosti 5, 2015 aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo, Juni 5, 2016 aliandika barua nyingine  ya kutengua barua yake ya kujiuzulu na kutangaza kurejea rasmi katika wadhifa wake huo.

Uamuzi huo ulikigawa chama na kuwa na pande ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na nyingine ikimuunga mkono Profesa Lipumba.

Licha ya kambi hiyo kumpinga, Msajili wa Vyama alitangaza kumtambua Profesa Lipumba akidai mchakato wake wa kujiuzulu ulikuwa hajakamilika kwa mujibu wa Katiba yao hadi alipoandika barua ya kutengua barua yake ya kujiuzulu.

Hivyo Msajili alisema kuwa licha ya kuandika barua hiyo ya kujiuzulu, lakini bado alikuwa ni mwenyekiti halali, kwani mamlaka iliyokuwa imemteua ambayo ni Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho, ilikuwa haijaridhia, kama katiba yao inavyoeleza.

Kutokana na uamuzi huo ndipo kambi ya Maalim Seif kupitia kwa baadhi ya wajumbe wa bodi waliokuwa upande wake ilifungua kesi mahakamani hapo ikidai kuwa Msajili hana mamlaka hayo kwani hayo ni masuala ya kiutawala ya ndani ya chama ambayo hawezi kuyaingilia.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016 walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na viongozi wengine 10 wanaomuunga mkono, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, ambaye pia ni mbunge wa Kaliua Tabora, Madgalena Sakaya.

Wanaiomba mahakama hiyo itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, wakidai kuwa hana mamlaka na imzuie kuingilia masuala ya ndani ya kiutawala ya chama hicho.

Wanadai kuwa Profesa Lipumba alishajiuzulu nafasi hiyo na Katiba ya chama chao haina utaratibu wa kiongozi kujiuzulu na kutengua tena uamuzi wake huo na kurejea katika nafasi hiyo na kwamba si mwanachama kwani alishavuliwa uanachama.

Lakini Profesa Lipumba na wafuasi wake huku wakiungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa wanadai kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CUF, ibara ya 117 (2) mchakato wa kujiuzulu kwake ulikuwa bado haujakamilika.

Wanadai kuwa ili uamuzi wa kujiuzulu ukamilie ni lazima mamlaka ya uteuzi wake (Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho) ukae na kuridhia barua yake ya kujiuzulu au kuikataa.

Wanadai kuwa hadi Profesa Lipumba anaandika barua ya kutengua barua yake ya kujiuzulu, hatua hiyo ilikuwa bado haijafanyika. Hivyo Profesa Lipumba alikuwa bado ni mwenyekiti halali wa CUF.