VIDEO: Mahakama yataifisha mali za Malkia wa Tembo, yampiga faini ya mabilioni

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka 15 kila mmoja washtakiwa watatu akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan(66), baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na  biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh13.9 bilioni


Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka 15 kila mmoja washtakiwa watatu akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan(66), baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na  baishara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh 13.9 bilioni.

Mbali na Glan, ambaye pia anajulikana kama Malkia wa meno ya Tembo, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 21/2014,  ni Salvius Matembo na Philemon Manase.

Mbali na kifungo hicho, Mahakama ya Kisutu imetaifisha nyumba na shamba  vyote vya mshtakiwa  Glan, iliyopo Muheza mkoani Tanga, ambavyo, vilihusika katika biashara ya meno ya tembo.

Pia Mahakama hiyo imewapiga faini ya Sh 27, 864, 000, 000, baada ya kupatikana na kosa la ununuzi na kusafirisha meno hayo 860 sawa na tembo wazima 430.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Februari 19, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi baada ya kuwatia hatiani, washtakiwa hao.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amedai katika shtaka la kwanza ambalo ni kujihusisha na mtandao wa uhalifu, ambao ni ukusanyaji wa meno ya tembo 860, kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 15 jela.

Katika shtaka la pili, ambalo ni kushiriki, kusaidia, kukusanya na kusafirisha meno ya tembo 860 yenye uzito wa kilo 15,900, washtakiwa kwa pamoja watatumikia kifungo cha miaka 15 kila mmoja.

Hakimu Shaidi, amesema katika shtaka la tatu ambalo ni kujihusisha na ununuzi na kusafirisha meno hayo 860 sawa na tembo wazima 430, kila mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh27, 864, 000, 000.

"Mahakama imewatia hatiani washtakiwa hawa kama walivyoshtakiwa, hivyo  adhabu hii inakwenda pamoja na kwamba washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja" amesema Hakimu Shaidi.

Baada ya Hakimu Shaidi kutoa hukumu hiyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Nehemia Nkoko akisaidia na Hassan Kiangio umesema kuwa wameweka  nia ya kukata rufaa.

Hatua hiyo inatokana upande wa mashtaka kupelekea mashahidi 11 ambao walitoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao, wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari Mosi,2000 na Mei 22, 2014.

Hadi kutolewa kwa hukumu hiyo, leo, washtakiwa hao wamekaa gerezani kwa muda wa miaka mitano.