Mahakama yazuia uchaguzi usifanyike jimbo la Joshua Nassari

Muktasari:

 

  • Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari amepeleka kesi ya maombi madogo ya kuomba kibali cha kufungua kesi ya msingi kwa ajili ya kutengua uamuzi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ya kumfutia ubunge wake.

 

  • Mei 14 Spika Ndugai alimuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi baada ya mbunge wake, Joshua Nassari kupoteza sifa za kuwa mbunge

Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imezuia kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo la Arumeru Mashariki hadi kesi ya maombi madogo ya kufungua kesi ya msingi ya kuomba kutengua uamuzi wa Spika wa kumfutia ubunge Joshua Nassari itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Akizungumza leo jijini hapa, naibu msajili wa Mahakama hiyo, Dayness Lyimo amesema kesi hiyo namba 22 ya mwaka 2019 inasikilizwa na Jaji Latifa Mansoor.

Amesema pia wajibu maombi ambao ni Spika na mwanasheria mkuu wa Serikali wamepewa siku saba kupeleka kiapo kinzani cha maombi hayo.

“Jaji pia ameagiza kusifanyike uchaguzi wowote (jimboni) hadi hapo maombi hayo yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” amesema.

Nassari ambaye alikuwapo mahakamani hapo asubuhi anawakilishwa na mawakili watu ambao ni Hekima Mwasipe, Jonathan Mndeme na Fred Kalonga.

Upande wa walalamikiwa unawakilishwa na wakili wa Serikali Masunga Kawahanda.

Kesi hiyo itakwenda tena mahakamani Machi 27 kwa ajili ya kusikilizwa.

Naye Nassari akizungumza na Mwananchi amewashukuru mawakili wake kwa hatua hiyo waliyofikia.

Mei 14  Spika wa Bunge, Job Ndugai alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu jimbo la Nassari liko wazi kutokana mbunge huyo kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge.