Mahitaji ya nishati yanavyopoteza misitu Tanzania

Muktasari:

Katika mfululizo wa makala zetu kuhusu matumizi ya mkaa na mazingira, leo tunaendelea kuangalia jinsi ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ulivyopoteza misitu mingi.

Nishati ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi. Kuna aina tofauti za nishati kama kuni, mabaki ya mimea, upepo, maji, nyuklia, jua, joto ardhi.

Ziko nyingine ambazo kabla ya kutumika zinatakiwa kuendelezwa.

Wakati nchi zilizoendelea hutumia kiasi kikubwa cha nishati kwa maendeleo ya viwanda, nchi zinazoendelea zinategemea zaidi mazao ya miti kuzalisha nishati ya matumizi ya kawaida.

Miti pia inakatwa na kuchomwa kwa matumizi mbalimbali kama vile kuimarisha matofali, kukausha tumbaku, kukausha samaki, kukausha chai, kutengeneza pombe za kienyeji na kupikia.

Tanzania, moja ya nchi zinazoendelea, hutumia asilimia 90 ya miti kuzalisha nishati, huku umeme ukichangia asilimia mbili na mafuta asilimia nane.

Matokeo yake yamekuwa ni uharibifu wa misitu kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na uchomaji wa mkaa.

Miongoni mwa sababu kubwa za uharibifu wa misitu ni mahitaji ya nishati. Taarifa za nishati nchini kwa mwaka 2010 hadi 2012 zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2011 ilikadiriwa kuwa asilimia 90.8 miti iliyovunwa Tanzania ilitumika kwa ajili ya nishati, hasa mkaa.

Mbali na mkaa, kuna mazao mengine ya mimea yanayotumika kama nishati ikiwa pamoja na kuni, mkaa, pumba za mchele, vumbi la mbao, randa, mabaki ya miwa iliyokamuliwa, maganda ya kahawa, korosho na mabaki ya mkonge.

Mbali na mimea, kuna nishati itokanayo na kinyesi cha wanyama na mabaki ya vyakula.

Biashara ya mkaa

Wakati nchi ikiendelea kuwa na eneo lilelile, idadi ya watu inaongezeka miaka hadi miaka na hivyo matumizi ya nishati hiyo yanazidi kukua, kwa mujibu wa Profesa Romanus Ishengoma, mtaalamu wa misitu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua).

“Tani milioni moja za mkaa zilitumika nchi nzima mwaka 2009 na kuongezeka hadi tani milioni 1.7 mwaka 2012 na zaidi ya nusu zimetoka katika mkoa wa Dar es Salaam,” anasema Profesa Ishengoma.

“Kati ya magunia 28,500 na 48,000 yamekuwa yakiingizwa Dar es Salaam kila siku kati ya mwaka 2009 hadi 2012. Biashara ya mkaa iliingiza Dola 650 milioni (za Kimarekani) kwa mwaka 2009 na bado uchomaji mkaa unaendelea kwa kasi,” anasema.  

Utengenezaji wa mkaa

Lakini hadi uweze kufanya biashara ya kiwango hicho, unakuwa umekata miti kwa kiasi kikubwa. Profesa Ishengoma anasema kuzalisha tani moja ya mkaa unahitaji kukata miti kati ya miti 10 na 12.

“Hadi mwaka 2012, hekta 583 za miti zilikuwa zinakatwa kila siku ili kuchoma mkaa. Zaidi ya familia 300,000 zimejiajiri katika kazi ya uchomaji mkaa na idadi hiyo imekuwa ikiongezeka,” anasema.

“Wazalishaji wengi wa mkaa hawana usajili wowote na hata baada ya kuzalisha, hakuna udhibiti wowote. Usafirishwaji wa mkaa hufanywa kwa njia mbalimbali ikiwa pamoja na pikipiki, baiskeli, magari ya watu binafsi na magari ya Serikali.”

Mbali ya Dar es Salaam anasema mkaa pia huuzwa Tanzania Visiwani na hata nje ya nchi.

Kazi ya mkaa inapuuzwa, athari kubwa

Profesa Ishengoma anasema kumekuwa na changamoto kubwa ya kudhibiti biashara ya mkaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa sheria imara, sera na kanuni madhubuti.

“Kazi yenyewe inachukuliwa kama ya kimaskini na isiyovutia. Matokeo yake inakosa udhibiti wa kutosha, wakati athari zake ni kubwa. Hakuna sera wala maono yanayoiunganisha kitaifa, japo zipo sheria,” anasema.

Anasema bado mkaa haujatambuliwa kama nishati ya kibiashara kama vile umeme, gesi na makaa ya mawe, badala yake unachukuliwa kama nishati ya jadi, ya chini na inayoharibu mazingira, kuliko kuchukuliwa kuwa nishati muhimu inayoweza kuendelezwa kwa masilahi ya Taifa.

Hata hivyo, Mkakati wa Pili wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (Mkukuta) wa Julai ulikuwa na maono ya kuibadili Tanzania kutoka kwenye nishati za kienyeji za miti kwenda kwenye nishati za kisasa.  

Awamu ya kwanza ya Mkukuta ilikuwa na malengo ya kupunguza uwiano wa watu wanaotegemea miti kama nishati, kutoka asilimia 90 mwaka 2003 hadi asilimia 80 mwaka 2010. Hata hivyo lengo hilo halikufikiwa.

“Tanzania ilipo sasa ni sawa na ilipokuwa Marekani miaka 160  iliyopita kwa kuwa haiwezi kuachana ghafla na matumizi ya miti kupata nishati, kwa kuwa gharama za nishati mbadala bado ni kubwa na Watanzania wengi hawana uwezo wa kuzimudu,” anasema Profesa Ishengoma.  

Profesa Ishengoma ameonya kama hakutakuwa na juhudi za makusudi za kupatikana kwa nishati mbadala na ya uhakika na kuongeza upandaji wa miti, uharibifu wa misitu utaongezeka maradufu.

“Upotevu wa miti unakadiriwa kuongezeka kutoka mita 19.5 za ujazo mwaka 2012 hadi kufikia mita 47.2 ifikapo mwaka 2030. Lazima kuwe na juhudi za kuweka nishati mbadala na sera zitakazounga mkono nishati endelevu,” anasema.

TFS yataka kudhibiti

Wakati upotevu wa miti ukikadiriwa kuongezeka, Taasisi ya Kusimamia Misitu (TFS) inajipanga kwenda kinyume, kama anavyosema mtendaji mkuu wake, Profesa Dos Santos Silayo.

“Kama umefuatilia vizuri nishati inayotumika kwa wingi nchini ni mazao ya miti, kwa hiyo hata tusipochukua ushuru wa mkaa haitasaidia kumaliza upotevu wa misitu. Isitoshe, ushuru huo ni asilimia 3 tu ya mapato yetu, kwa hiyo siyo kwamba tunategemea sana,” anasema Profesa Silayo.

Alisema kwa upande mwingine ushuru huo ni njia mojawapo ya kudhibiti ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa.

Amesema njia nyingine za udhibiti ni kushawishi wadau wengine kuharakisha kugundua vyanzo vingine vya nishati kama utengenezaji wa mkaa mbadala kwa kutumia vumbi la mimea na matumizi ya gesi asilia na gesi za mafuta.

“Mpaka sasa kuna hoteli kubwa Dar es Salaam zinatumia mkaa mbadala na kuna shule nyingi zinatumia mkaa huo jijini Dodoma. Tunadhibiti pia kule mkaa unakotoka, kama tulikuwa tunatoa vibali 10 vya kuchoma mkaa, sasa tutatoa vitano,” anasema Profesa Silayo.

Wadau wa nishati mbadala

Wakati njia mbadala za upatikanaji wa nishati zikitafutwa, baadhi ya wadau wanasema wanalazimika kuuza nishati mbadala bei ghali kutokana na ubora wa vifaa vyao.

Meneja masoko wa kampuni ya Mobisol, Seth Mathemu amesema gharama za huduma za umeme jua zinatokana na ubora wa huduma wanayotoa.

“Mpaka sasa tumeunganisha kaya 90 nchi nzima ambazo ni sawa na watu 450,000 kwa wastani wa kaya moja kwa watu watano. Bado watu wengi wanahitaji huduma hizo, lakini wanalalamikia gharama. Gharama zetu ni kutokana na huduma bora tunayotoa,” anasema Matemu.  

Mkurugenzi wa miradi na biashara wa kampuni ya Ensol, Prosper Magali anasema uwekezaji wa miradi ya nishati mbadala inakuwa migumu kwa sababu ya mabadiliko ya mikataba waliyoingia na Serikali.

“Kuna wawekezaji wengi wa umeme mbadala walishaingia mikataba na Serikali, lakini sasa wamebadilishiwa bei. Kwa mfano unakuta mwekezaji alisema atauza umeme kwa senti 12 za doka la Kimarekani kwa uniti, halafu Serikali inataka auze kwa senti 4.5, kwa wengi wanashindwa,” anasema Magali.