Majaliwa: Eid itumike kuwakumbuka yatima, wajane

Muktasari:

Waislam wametakiwa kutumia sikukuu ya Eid El Fitr kutenda matendo mema na kuwakumbuka yatima kama walivyokuwa wakifanya wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhan

Dar/Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Waislamu nchini kuitumia sikukuu ya Eid el Fitr kwa kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.

Pia amewasisitiza kuimarisha ushirikiano na mashikamamo miongoni mwa Waislam na madhehebu mengine huku wakihakikisha wanayaendeleza mambo mema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatano Juni 5, 2019 wakati aliposhiriki swala ya Eid El Fitr katika msikiti wa Anwar uliopo Msasani jinini Dar es Salaam.

“Leo ni siku kubwa na muhimu kwa Waislamu (ambao) wanahitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea siku kuu ya Eid El Fitr, hivyo tuendeleze matendo mema.”

“Tumeona utulivu uliojitokeza katika mwezi mtukufu na jambo hili limesisitizwa na viongozi wa dini. Tuendelee kuwa wamoja, tuimarishe mshikamano na tuvumiliane,” amesema Majaliwa

Pia, Waziri Mkuu amewakumbusha wazazi na walezi kuwaongoza watoto kwa kuwapa mafundisho ya dini yatakayowawezesha kumjua Mwenyezi Mungu na kuwa raia wema.

Akitoa mawaidha Imamu wa msikiti huo, Sheikh Mhina amesema Waislamu wanatakiwa kuitumia siku ya leo kwa kuhamasisha amani pamoja na kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo.

 Pia amewasisitiza wayaendeleze mema yote waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu na kuwajali wazazi wao.

 

Sheikh wa Dodoma

Sheikh wa mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amewataka Waislamu kutowatelekeza watoto yatima na kuwafanya warudi katika simanzi na majonzi badala yake waendelea kuwa karibu nao kama ilivyokuwa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 

Ameyasema hayo wakati akitoa ujumbe wa Siku Kuu ya Eid katika msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma leo Jumatano na kusema katika kipindi cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani hakuna mtoto yatima aliyesikitika na kuachwa mwenyewe.

“Katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani hakuna aliyemuacha mtoto yatima tulikuwa nao pamoja sasa hii isiishie hapo tunatakiwa kuwa nao hata miezi mingine.”

“Tusiwafanye hawa watoto kuwa wanyonge, wapweke, mpaka wakajihisi hali ya tofauti, ni wenzetu hivyo tunatakiwa kuendelea kuwatoa kwenye hali ya majonzi na simanzi,” amesema Sheikh Rajab.

Hata hivyo, amesema kwa Waislamu wapo ambao baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuisha watarudia kufanya yale waliyokuwa wakiyafanya kipindi cha nyuma.

“Wengi walikuwa wanahisi wamefungwa sasa leo wanasema wamefunguliwa na hapo wanafurahi kwelikweli ili wakafanye na mambo yao ya uasherati. Matukio mengine ambayo ni mabaya, acheni tabia hiyo tuishi maisha yale tuliyokuwa tunaisha wakati tumefunga,” amesema.

Aidha amewataka wananchi kwa ujumla kuacha tabia ya kuhamasisha vitendo vya kufanya mambo mabaya ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu.

Amesema maisha ambayo Watanzania wanatakiwa kuishi maisha ya kutobaguana kwa sababu ya dini au kabila, akisema katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani  hata wale ambao si Waislamu walishiriki kwenye matukio ya kufuturisha, ikiwa ni ishara ya kuonyesha Watanzania ni kutu kimoja.