Majaliwa: Wageni SADC waje kuwekeza viwanda Tanzania

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi wakionyesha bango la Mkutano wa Sadc alipotembelea mabanda kwenye maonyesho ya nne ya wiki ya viwanda kwa nchi za Sadc yanayoendelea jijini Dar es Salaa Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuunganisha nguvu ya pamoja itakayosaidia kuanzisha viwanda vya bidhaa hapa nchini kwa kushirikiana na wafanyabiashara wageni kutoka nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa nchi hiyo kuunganisha nguvu ya pamoja itakayosaidia kuanzisha viwanda vya bidhaa hapa nchini kwa kushirikiana na wafanyabiashara wageni kutoka nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC).

Pamoja na wito huo, Majaliwa ameagiza kila Mtanzania anakuwa balozi wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania bara na Visiwani kwa wageni wanaoshiriki maonyesho ya bidhaa katika wiki ya Viwanda kwa nchi 16.

Tayari wafanyabiashara wageni 172 kati ya 1,576 wa nchi 16 za Jumuiya hiyo wamejitokeza kuanzia jana Jumatatu kuanza kutangaza bidhaa zao kwa lengo la kukuza mtandao wa masoko ya Nchi za SADC kupitia bidhaa zake.

Kwa mujibu wa wizara ya viwanda, tayari washiriki 3,001 wameshajisajili kushiriki mikutano ya SADC, wakitokea nchi za SADC ikiwamo Tanzania.

Akizungumza leo Jumanne Agosti 6, 2019 katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Majaliwa amesema, “Tuwakaribishe kwa ukarimu na tuwapeleke katika maeneo ya vivutio vya Tanzania, kuna mlima Kilimanjaro, fukwe za bahari, wengine wanasema mlima Kilimanjaro ni mali yao, “amesema Majaliwa.

“Lakini pia tunawakaribisha wafanyabiashara wanaoweza kuungana na watanzania waanzishe viwanda hapa Tanzania, ni fursa ya kukuza mtandao wa masoko ya bidhaa za Tanzania, kwa hiyo tutumie fursa hii,” amesema Majaliwa akisisitiza ukarimu kwa wageni hao.

Maonyesho hayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2016 nchini Eswatini, mwaka 2017 nchini Afrika Kusini , mwaka 2017 nchini Namibia na awamu ya nne mwaka huu nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza 2015/30 ya Mkakati wa Viwanda wa SADC 2015/2063.

Akiwa JNICC, Wazir Majaliwa ametembelea mabanda mbalimbali ya wafanyabiashara wa Tanzania, akipongeza ubora wa bidhaa zinazoweza kuteka soko la nchi za SADC.