Majaliwa aagiza walinzi kukamatwa

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza walinzi waliokuwa lindo eneo la ujenzi wa stendi ya kimataifa ya mabasi ya Ngangamfumuni siku ulipotokea wizi wa tani tano za nondo kukamatwa

 


Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza walinzi waliokuwa lindo eneo la ujenzi wa stendi ya kimataifa ya mabasi ya Ngangamfumuni siku ulipotokea wizi wa tani tano za nondo kukamatwa.

Ametoa agizo hilo leo Alhamisi Julai 18, 2019 alipotembelea mradi wa ujenzi huo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Amedai ni aibu Serikali kutenga fedha kwa ajili kutekeleza miradi ya maendeleo halafu wanajitokeza wacheche na kuihujumu.

Majaliwa amesema endapo  walinzi hao hawatapatikana, viongozi wa kampuni husika wakamatwe ili kutoa ushirikiano wa sehemu walipo wafanyakazi wao.

"Wananchi wa Moshi mmetukatisha tamaa, kumeibuka tabia ya wizi wa vifaa vya ujenzi hapa. Naelezwa zimeibiwa Nondo tani Tano.”

“Walinzi waliokuwa lindo siku hiyo wasakwe popote walipo wakamatwe kwa sababu hauwezi kuchukuliwa mzigo mkubwa kama huo na wao wasijue," amesema Majaliwa.

Mtendaji mkuu huyo wa Serikali ya Tanzania ameutaka uongozi wa manispaa ya Moshi kuweka utaratibu mzuri wa ulinzi wa vifaa vya ujenzi wa mradi huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah amemueleza Majaliwa kuwa walinzi waliokuwa zamu  walikimbia na polisi wanawasaka ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Ujenzi wa stendi hiyo unatarajiwa kufanyika kwa miezi 24, Serikali imetenga Sh9 bilioni.