Majaliwa aagiza kufungwa kwa masoko nje ya kambi za wakimbizi

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameamuru kufungwa kwa masoko ya muungano yaliyopo nje ya kambi za wakimbizi mkoani Kigoma kutokana na kuwa chanzo cha uhalifu wa kutumia silaha za kivita


Kibondo. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameamuru kufungwa kwa masoko ya muungano yaliyopo nje ya kambi za wakimbizi mkoani Kigoma kutokana na kuwa chanzo cha uhalifu wa kutumia silaha za kivita.

Akizungumza leo Jumanne Februari 19, 2019 na watumishi wa idara mbalimbali wilayani Kibondo mkoani humo, Majaliwa amesema wakimbizi wanatakiwa kukaa kambini na kama kuna haja ya kuwa na soko la pamoja masoko hayo yaanzishwe ndani ya kambi na Watanzania wanaoingia wafuatiliwe.

Amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na kushirikiana na wananchi kudhibiti uhalifu ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika kwa amani.

Majaliwa pia amekemea kitendo cha wananchi kuvaa sare za kijeshi za nchi yoyote kama sio wanajeshi, akisisitiza kuwa atakayebainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Kaimu mkuu wa kambi ya wakimbizi ya Nduta, Barnabas Kipi amesema wakimbizi 250 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kutoka nje ya kambi bila vibali.