Majaliwa aridhishwa na miradi inayotekelezwa jimboni kwake

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na hospitali ya wilaya hiyo. Majaliwa yuko Ruangwa kwa mapumziko mafupi huku akitembelea miradi ya maendeleo jimboni kwake.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa Ruangwa yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi na jana Jumatatu Julai 29,2019 alikagua ujenzi huo unaohitaji Sh3.77 bilioni hadi kukamilika kwake na kutekelezwa na Suma JKT.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema ofisi hiyo itakuwa na ghorofa moja na ujenzi wake ulianza Juni Mosi, 2019 na unatarajiwa kukamilika Julai 2020. Jengo litakuwa na ofisi 33 za chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.

Akiwa kwenye eneo la ofisi hizo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba halmashauri hiyo imepokea Sh500 milioni kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya halmashauri hiyo.

Akizungumza na wakazi waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Majaliwa aliwapongeza viongozi wa halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua kutumia ‘force account’ ambayo alisema inapunguza gharama za manunuzi.

Majaliwa aliitaka halmashauri hiyo isisubiri hadi kazi ya ujenzi ikamilike na badala yake wahusika wajipange na kuanza kufanya usafi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo. 

“Halmashauri tusikae tu kusubiri ujenzi uishe. Tufanye usafi kuzunguka eneo lote, tupande miti na maua ili mandhari ianze kupendeza,” alisema Majaliwa

Kuhusu muda wa kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu aliwashauri mafundi wazidishiwe muda wa kufanya kazi. “Badala ya kufanya kazi mchana peke yake, bora waongezewe muda wafanye hadi usiku ili kufidia muda uliopotea na uliobakia ni mfupi mno.”

Kazi ambazo zimeshafanyika hadi sasa ni usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi; upimaji wa sampuli ya udongo (Geotech Survey); uingizaji wa maji eneo la ujenzi; uchimbaji wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji  na uvutaji wa umeme eneo la ujenzi.

Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000 yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya matofali yote. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi unaendelea.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Mahela Njile alisema kwamba hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa kugharimu Sh7.5 bilioni kulingana na makisio ya Ofisi ya Rais - Tamisemi.

Dk Njile alisema katika awamu ya kwanza Serikali imetoa Sh1.5 bilioni na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.