Majaliwa asisitiza malipo ya korosho yakamilike Januari

Thursday January 17 2019

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kubadilisha mfumo wake wa malipo ili iweze kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa.

Alisema ametoa agizo hilo baada ya Serikali kuendelea kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu suala la malipo wakati kwa kawaida malipo ya mkupuo hukamilika ifikapo Januari 10 ya kila mwaka.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu ilieleza kuwa agizo hilo alilitoa jana wakati akizungumza na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na mkurugenzi mkuu wa TADB, Japhet Justine kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video kutokea ofisini kwake mjini Dodoma.

“Matarajio yetu yalikuwa ni kuvuna tani 245,000 au zaidi kidogo, lakini umesema hadi sasa korosho zilizo kwenye maghala ni tani 206,000 maana yake takriban tani 40,000 ziko Amcos au majumbani kwa wakulima. Na ambazo mmezilipia hadi sasa ni tani 92,000 na pointi zake. Tuko chini ya nusu,” taarifa hiyo inamkariri Majaliwa.

“Hili zoezi la uhakiki na malipo, lilianza Novemba 27, 2018 na leo ni tarehe 16 Januari, 2019 na hatujafika hata asilimia 50, maana yake zoezi hili tutalimaliza Aprili mwanzoni. Haiwezekani. Tunapata lawama kutoka kwa wakulima wa korosho kwa sababu hii kasi ni ndogo; na haya siyo malengo ya Mheshimiwa Rais, aliyetaka korosho zinunuliwe na Serikali.”

Pia Waziri Mkuu alihoji sababu za benki hiyo kutoshirikiana na vyama vikuu au vyama vya msingi ili kubaini idadi halisi ya wakulima na idadi kamili ya kiasi walichovuna kwa sababu kila chama cha msingi kina wanachama wanaojulikana. “Zao la korosho lina mfumo wa ushirika. Amcos ziko kwenye ngazi ya vijiji na unaweza kukuta Amcos moja ina wanachama zaidi ya 200, sasa bila kupitia kwenye hizi Amcos unawezaje kujua kila mkulima amevuna kilo ngapi na anadai kiasi gani kwa kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee?” alihoji.

“Kwa nini msitumie mfumo huo lakini mkawatenga kwenye makundi mawili yaani wakulima wenye chini ya kilo 1,500 au zaidi ya 1,500 ili muweze kufanyia uhakiki kwa urahisi?”

Waziri Mkuu pia aliwataka wakuu wa mikoa hiyo wahuishe taarifa zao na wamtumie ili aweze kuzitumia kuratibu zoezi zima na kwamba amefanya mazungumzo na wakurugenzi wa benki za CRDB na NMB na kuwasisitiza kuwa suala la miamala ya malipo ya korosho lifanywe mchana na usiku ili malipo yakamilike kabla ya Januari mwishoni .


Advertisement