Majaliwa ataka Ruvuma kutangaza fursa za uwekezaji

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma kuendelea  kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa vikwazo ili kuvutia wawekezaji zaidi.

Songea. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma kuendelea  kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa vikwazo ili kuvutia wawekezaji zaidi.

 “Mkoa wa Ruvuma kama ilivyo mikoa mingine unazo fursa ambazo zikiendelezwa zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Nitoe rai kwa mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje,” amesema Majaliwa. 

Ametoa wito huo leo jana Alhamisi Julai 25, 2019 wakati akifungua kongamano la biashara na uwekezaji mkoani Ruvuma kwenye uwanja wa Majimaji manispaa ya Songea. Pia amezindua mwongozo wa uwekezaji wa mkoa huo.

Amesema katika ustawi wa uchumi, nchi nyingi duniani zimeweza kukuza uchumi kupitia ujenzi wa viwanda na zikafanikiwa kupunguza umasikini katika jamii zao. Amezitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, China, Japani, Korea ya Kusini na Ujerumani.

“Tunapaswa kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo maana Tanzania pia tunahamasisha ujenzi wa viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa ili tulete mageuzi ya kiuchumi yatakayowezesha upatikanaji wa ajira na hatimaye kuondoa umaskini.”

“Kongamano hili ambalo kauli mbiu yake ni ‘Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda, wekeza sasa’, imelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani humu, na  ina jipambanua vema na kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025,” amesema Majaliwa. 

Amesema mchango wa sekta ya viwanda kiuchumi na kijamii nchini ni pamoja na kuongeza pato la Taifa na kupandisha hali ya maisha ya wananchi.

Nyingine ni usaidia nchi isiyumbe kiuchumi ikizingatiwa kuwa viwanda vingi havitegemei hali ya hewa kama kilimo, kuboresha urari wa biashara  kwa sababu tija yake ni kubwa na hasa zikiuzwa bidhaa nyingi nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amezitaja faida nyingine kuwa ni kuchangia maendeleo ya sekta nyingine kama za kilimo, uvuvi, elimu na madini, kutengeneza ajira kwa wananchi, kuchagiza na kuharakisha maendeleo ya teknolojia na rasilimali watu na kuwezesha matumizi mazuri ya maliasili zilizopo kwa faida zaidi.

Amesema nyingine ni  kuleta uhakika wa soko la mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa sababu hutumika kama malighafi na kuwepo kwa uhakika wa kuingiza fedha za kigeni nchini kupitia mauzo ya bidhaa nje ambapo husaidia kuagiza mitambo, malighafi na bidhaa nyingine ambazo hazizalishwi nchini.

Awali, kitoa salamu kwa niaba mabalozi wengine, mwakilishi wa balozi wa China, Xian Bing amesema ana uhakika kongamano hilo litafanikiwa kuleta mabadiliko mkoani humo kwa sababu wana bidii ya kazi.

“Ninaahidi kuleta wawekezaji kutoka China kwa sababu tunataka waje kuleta teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na Watanzania na wawafundishe teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma iwe model (mfano) kwa mikoa mingine,” amesema.