Majaliwa ataka Watanzania kudumisha amani, kuliombea Taifa

Muktasari:

Watanzania wametakiwa kutumia mwezi mtukufu wa Ramadhan kudumisha amani na kuwaombea viongozi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuutimia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kudumisha amani na mshikamano na kuwaombea viongozi wa kitaifa.

Amesema kila mwananchi aendelee kuliombea Taifa lizidi kudumisha amani na mshikamano.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Mei 25, 2019 na ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa kiongozi huyo alitoa kauli hiyo jana jioni Ijumaa Mei 24, 2019 aliposhiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NMB.

“Mwezi huu tuna majukumu makubwa ya kufanya ibada, kutubu dhambi zetu na kuomba rehema kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kudumisha mshikamano na kuwa wavumilivu.”

“Tuhakikishe tunatenda matendo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu,” amesema.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza NMB kwa huduma bora wanazozitoa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwa na matawi mengi hadi vijijini.

Mkurugenzi wa benki ya NMB, Albert Jonkergouwa amesema lengo la kuandaa hafla hiyo ya futari ni kuimarisha ushirikiano uliopo baina yao na wateja wao.

Jonkergouwa amesema katika kipindi hiki Waislamu wanapaswa kumrudia muumba wao na kumshukuru kwa mema yote anayowajalia waja wake.

“Mwezi wa Ramadhan ni kipindi muafaka cha kufuturu pamoja hivyo nawashukuru wateja wetu kwa kujumuika nasi nawaomba muendelee kutumia huduma zetu.”

Amesema mkusanyiko huo unadhihirisha kuwa wao ni sehemu ya jamii ya Watanzania wote, hivyo aliwasisitiza wateja wa benki hiyo waendelee kutumia zaidi huduma za kidijitali.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, mashekhe wa mikoa ya kanda ya kati,  wabunge ,viongozi wa dini, wananchi, wazee wa Dodoma, wawakilishi wa taasisi mbalimbali na wafanyakazi wa NMB.