Majaliwa ataka Wizara ya Michezo kumaliza tathmini ya shule 56

Monday June 10 2019Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa 

By Haika Kimaro, Mwananchi [email protected]

Mtwara. Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ameiagiza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na ofisi ya Rais Tamisemi kukamilisha tathmini ya shule 56 za serikali zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya michezo nchini ili kupata ufahamu wa njia bora zaidi na kuongeza vipaji ikiwa ni pamoja na kushirikisha makundi yote wakiwamo wenye ulemavu.

Akizungumza katika  ufunguzi wa mashindano ya Umitashumta na Umiseta yanayofanyika kitaifa mkoani Mtwara amesema shule hizo zilifadhiliwa na taasisi iliyokuwa Mtwara na kufundisha walimu wengi wa michezo pamoja na kila mkoa kuwa na shule ya michezo kuimarisha michezo.

Pia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurudisha na kuimarisha mchepuo wa michezo katika Chuo cha Ualimu Butimba ili kupata wataalamu zaidi wa michezo ikiwa ni pamoja na vyama vya michezo kitaifa kuhakikisha vinapeleka wataalamu wake katika mashindano hayo ili kushirikiana na wizara kugundua vipaji na kupata wachezaji mahiri.

“Lakini pia halmashauri endeleeni kuwaruhusu walimu mbalimbali nchini kuhudhuria mafunzo ya michezo katika chuo cha maendeleo ili kupunguza uhaba wa walimu wa michezo katika halmashauri ,”amesema Majaliwa.

Ameitaka wizara husika kuona umuhimu wa kurudisha mashindano ya vyuo vya ualimu Umisavuta ili kuwa na mwendeleo mzuri katika kukuza vipaji kwa walimu.

“Umisavuta  ni kwa walimu, Umitashumta ni wanafunzi wa shule za msingi na Umiseta ni wanafunzi wa sekondari, kwa hiyo tukiimarisha michezo kwa walimu wanapokwenda kufundisha watasimamia michezo. Wanacheza Umitashumta na Umiseta, lakini huku Umisavuta hakuna kitu, natamani mwakani kupata taarifa ya maandalizi ya michezo hiyo,”amesema Majaliwa.

Advertisement

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema mashindano hayo kwa mwaka huu yatawaweka pamoja  wanamichezo na viongozi  mbalimbali zaidi ya 6,500 ambao watakuwa mkoani Mtwara kwa kipindi chote cha mashindano.

“Napenda kuwahakikishia viongozi na washiriki wote ulinzi na usalama wakati wote wa mashindano na watapata huduma zote za msingi, Mkoa wa Mtwara umejiandaa kushinda  na sio kushiriki na kwa washiriki wengine kuweni macho,”amesema Byakanwa.

Advertisement