Majaliwa atoa angalizo uandikishaji Daftari la Wapigakura

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wanaoandikisha wananchi katika Daftari la Wapigakura kufanya kazi kwa weledi na kuepuka kujihusisha na siasa

Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wanaoandikisha wananchi katika Daftari la Wapigakura kufanya kazi kwa weledi na kuepuka kujihusisha na siasa.

Amewataka wahakikishe wanatumia lugha nzuri na kujituma wakati wa uandikishaji kwa kuzingatia kanuni na mwongozo utakaotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 18, 2019 katika uzinduzi wa uboreshaji wa daftari hilo kwenye viwanja vya

Mandela manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema ni jukumu la watendaji hao kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa waledi ili kufanikisha uandikishaji huo muhimu kwa Taifa unaolenga kupunguza malalamiko.

"Katika uandikishaji mtendaji huna haja ya kujua anayetaka kujiandikisha anatoka chama gani ili mradi yeye ni Mtanzania suala la chama atajua mwenyewe.”

“Tunajua katika hili hatuwezi kuwa wakamilifu kwa asilimia 100 yale madogo yatakayojitokeza tuendelee kuzungumza. Tume iko  wazi hamna haja ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari waoneni wahusika wamalize jambo hilo,” amesema Majaliwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenister Mhagama amesema baada ya uandikishaji kukamilika, NEC  itatoa fursa ya wananchi, kuhakiki taarifa zao kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.