Majaliwa atoa neno kwa wanaume kupima afya

Muktasari:

  • Wanaume wametakiwa kwenda kupima afya zao na kuacha kutegemea matokeo ya wake zao wanapopima na kubainika wako salama hufurahia matokeo hayo bila kujua kwamba  yawezekana wakawa si salama

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wanaume kwenda kupima afya zao na kuacha kutegemea matokeo ya wake zao kushangilia pindi wanapobainika wako salama.

Majaliwa ametia wito huo leo Jumatano Juni 5, 2019 katika maadhimisho ya Baraza la Eid El Fitr lililofanyika Hoteli ya Tanga beach resort Mkoa wa Tanga ambapo amemwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Amesema wanaume waache kutegemea vipimo hivyo ili kuhakikisha lengo la asilimia 90 la Watanzania wote kufanya vipimo ifikapo mwaka 2020 liwe limetimia.

“Tunafanya hivi kwa sababu maambukizi yake yanakuja katika namna tofauti siyo moja, kwa hiyo kajiridhishe kuwa je namna zote hizo uko salama,” amesema Majaliwa.

Amesema Ukimwi unamaliza nguvu kazi ya Taifa hivyo hawawezi kuendelea kusita kutamka athari za ugonjwa huo kama viongozi wenye dhamana kwa sababu ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo.

“Tukifanikiwa kusimama kwa pamoja katika vita hii tutafanikiwa kuokoa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya kesho katika Taifa kwa sababu maambukizi kwao yanaongezeka na wanaweza kuingia katika kundi hilo bila kujua,” amesema

Amesema viongozi wanapaswa kusema jambo hilo kwa waumini wao kwa uwazi ili kuhakikisha kuwa kampeni ya ‘90,90,90’ iliyoanzishwa na Serikali inafanikiwa hadi mwakani.

Amesema hiyo ni moja kati ya kampeni nyingi zilizoanzishwa na Serikali huku akibainisha kuwa nyingine ni ile ya kupiga vita rushwa ili kuleta maendeleo.

“Lakini pia tuna kampeni za usafi katika mazingira yetu ili kuepuka magonjwa ya mlipuko, hakikisheni wenza wenu wanazingatia usafi katika mazingira yanayowazunguka na leo tumeshuhudia mifuko ya plastiki ilivyokuwa mingi katika kila mitaro jambo ambalo lilikuwa linazuia maji kwenda,” amesema Majaliwa.