Majaliwa awatuliza Kigoma, awaonya watumishi wazembe

Saturday July 13 2019

Waziri Mkuu wa Tanzania,Kassimu Majaliwa,mkoani Kigoma, ziara ya kikazi,

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassimu Majaliwa 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa amesema Serikali ya nchi hiyo haijawatupa wananchi wa mkoa wa Kigoma na kwamba inawakumbuka na ndiyo maana wamekuwa wakipelekewa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Pia, Majaliwa mkakati wa Serikali ya Tanzania ya kuwaondoa kazini watumishi wa umma ambao ni wazembe, wala rushwa na wasiotimiza majukumu yao ipasavyo ni endelevu hivyo kuwataka kuzingatia sheria na kanuni za utumishi.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 13, 2019 wakati akiongoza Kongamano la Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) la kumpongeza na kumuombea Rais wa Tanzania, John Magufuli ambalo limefanyika viwanja vya Lake Tanganyika.

Amesema Serikali inawakumbuka na ndiyo maana imeendelea kuwasogezea huduma muhimu.

Amesema mkoa wa Kigoma ni mkoa wa kimkakati na kwamba tayari Serikali imeleta fedha za huduma za afya kwaajili ya kununua vifaa tiba, dawa pamoja na vitenganishi ambapo kwa wilaya ya Kibondo imepokea Sh956 milioni.

Majaliwa amesema wilaya ya Kakonko imepokea Sh621 milioni, wilaya ya Uvinza Sh773 milioni, Kasulu Sh721 milioni, halmashauri ya wilaya ya Kigoma Sh829 milioni huku manispaa ya Kigoma Ujiji imepokea Sh651 milioni.

"Serikali inawakumbuka na haijawaacha nyuma kama mnavyosema kwa kutumia kauli ya wao wamekuwa wa mwisho kimaendeleo," amesema Majaliwa

Kuhusu watumishi, Majaliwa amsema, “Serikali inahitaji watumishi wenye heshima na nidhamu ya kazi ili waweze kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote iwe wa kiuchumi, kidini au kikabila.”

"Watumishi wa umma tunataka watambue kwamba wao ni watumishi wa wananchi, hivyo hawana budi kutambua wajibu wao ambao ni kuwatumikia mwananchi ipasavyo."

Amesema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya rushwa ambapo kwa Afrika Tanzania inaongoza kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Transparency Internation.

Awali, Katibu Mkuu wa UWT, Queen Mlozi amesema kongamano hilo ni mwendelezo wa makongamano mengine ya kumpongeza Rais Magufuli yaliyofanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Unguja na Pemba.

Amesema viongozi hao wameonesha dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo, "Tutaendelea kushirikiana na viongozi wetu na hatupo tayari kugawanyika."

Waziri Mkuu Majaliwa yupo mkoani Kigoma kwa ziara kuangalia maendeleo na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015/20.

 


Advertisement