Majaliwa azionya asasi za kiraia, wananchi

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amezindua shughuli ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura huku akitumia fursa kilo kutoa onyo kwa wananchi kutokujiandikisha mara mbili pamoja na asasi za kiraia kutokugeuka wasemaji wa vyama vya siasa.


Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaonya wananchi kuepuka kujiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja na kusema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 18, 2019 wakati akizindua uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapigakura katika viwanja vya Mandela, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema wananchi wenye sifa wanapaswa kujitokeza kwenye vituo kujiandikisha na wakishajiandikisha kwenye kituo kimoja hawataruhusiwa kujiandikisha kituo kingine.

"Hairuhusiwi mwananchi kujiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja na ukithibitika kuna mtu anayejiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, tutawakamata," amesema Majaliwa  

Aidha waziri mkuu ametumia pia nafasi hiyo, kuzionya asasi za kiraia zilizopewa fursa ya kutoa elimu, kuepuka kuvisemea vyama vya kisiasa na badala yake kufanya kazi hiyo kwa weledi na kwa kuzingatia taratibu za tume ya taifa ya uchaguzi.

"Rai yangu asasi za kiraia msijihusishe na kuzisemea chama chochote cha kisiasa wakati wa kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la wapiga kura, toeni elimu kwa kujibu wa sheria ili kuondoa malalamiko," amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage amesema shughuli hiyo ya uboreshaji wa daftari la mpiga kura ni hatua muhimu kwa tume hiyo katika kupata takwimu za wapiga kura kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchaguzi mkuu mwaka 2020.