Majaliwa azitaka benki kutafakari riba

Muktasari:

  • Akizindua tawi la Benki ya CRDB lililopo katika jengo la LAPF mjini Dodoma, Desemba 13, 2017, Rais Magufuli alizitaka benki kupunguza riba kwa kuwa imekuwa changamoto inayosababisha wateja wengi kushindwa kurejesha mikopo na wengine kuogopa kukopa.

Mwanza. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na Rais John Magufuli kuzitaka benki zipunguze riba ya mikopo ili kuwawezesha wananchi wakiwamo wakulima kukopa.

Akizindua tawi la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Tadb) mjini Mwanza jana, Majaliwa alizitaka taasisi hizo za fedha kuangalia upya na kutathmini riba wanazotoza kwa wateja kwa kuwa ni kubwa na hazilengi kuwanufaisha watu wa hali ya chini.

“Nenda mpunguze riba zenu, wananchi wengi wanaogopa kuzisogelea benki wanaziona kama kituo cha polisi, Serikali tusingependa kuona hilo likiendelea, lazima tuwawezeshe wakulima ili waone kama kilimo ni kimbilio kwao,” alisema.

Akizindua tawi la Benki ya CRDB lililopo katika jengo la LAPF mjini Dodoma, Desemba 13, 2017, Rais Magufuli alizitaka benki kupunguza riba kwa kuwa imekuwa changamoto inayosababisha wateja wengi kushindwa kurejesha mikopo na wengine kuogopa kukopa.

“Mkifanya hivyo mtafungua milango kwa wateja wengi, kwani watajitokeza kukopa jambo ambalo litachochea kukua kwa sekta binafsi nchini na hivyo kusababisha uchumi wa Taifa letu kukua kwa kasi tunayoitarajia,” alisema Rais.

Mkurugenzi mtendaji wa Tadb, Japhet Justin alisema hadi kufikia Februari benki hiyo imefikia mtaji wa Sh68 bilioni.

Alisema kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 13 ya Sh60 bilioni walizopewa na Serikali mwaka 2015 walipoanza kufanya kazi rasmi.

“Mpaka sasa tumeshatoa mikopo yenye thamani ya Sh107 bilioni,” alisema Justin.