Majaliwa azitaka sekta za fedha ziwe imara

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefungua Ofisi Ndogo na Tawi la Benki ya Biashara ya (TIB) jijini Dodoma huku akitoa wito kwa taasisi za fedha kusogeza huduma hizo kwa wananchi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema sekta ya fedha inapaswa kuwa imara na kuhakikisha huduma zake zinawafikia wananchi wengi katika maeneo ya mijini na vijijini ili iweze kutoa mchango unaokusudiwa katika kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa jamii. 

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu, Juni 24, 2019 wakati alipofungua Ofisi Ndogo na Tawi la Benki ya Biashara ya (TIB) jijini Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha ofisi yake imemnukuu Waziri Mkuu akisema ukuaji wa sekta ya huduma za kifedha ni muhimu sana katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Amesema benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi, hivyo, benki zinatakiwa kuzingatia mahitaji ya wananchi, kuwahamasisha na kuwaelimisha umuhimu wa kutumia benki. 

“Wananchi nao pia wana wajibu wa kuzitumia benki hizi kwa kutunza akiba zao na kukopa wakati wanapohitaji kuwekeza kwa malengo yaliyokusudiwa. Suala la msingi ni kuwa mnapokopa mkumbuke pia kurejesha kulingana na makubaliano.” 

“Sifurahishwi sana na takwimu zinazoonesha kwamba ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania wote ndiyo wanaopata huduma za kifedha kupitia mifumo halali ya kibenki, huku asilimia 48.6 wakipata huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu na asilimia 35 ya waliosalia kutopata kabisa huduma rasmi za kibenki,” amesema  

Waziri amesema hali hiyo haikubaliki kwenye nchi kama Tanzania ambayo inakabiliana na ujenzi wa uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo ametoa wito kuwa benki zote ziendelee kubuni mikakati na mbinu zitakazowawezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki tena kwa gharama nafuu ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua kutoka kwenye umaskini. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema tozo za mabenki kwa wateja bado ni kubwa na haziwasaidii wananchi wa kawaida, kwa hiyo, zipunguzwe, “Riba kwa wakopaji nazo ziko juu sana ukilinganisha na mfumuko wa bei, pia nazo zipunguzwe.”

Kuhusu changamoto ya riba kubwa inayotozwa kwa mikopo ya benki, Majaliwa amesema tayari Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imefanikiwa kupunguza riba ya hati fungani za Serikali, pamoja na ile inayotozwa kwa mabenki yanayokopa Benki Kuu. Moja ya lengo la kufanya hivyo ni kutaka riba za mabenki zipungue. 

 

“Naomba mabenki yaunge mkono jitihada hizo za Serikali kwa kupunguza riba zinazotozwa hasa kwenye mikopo ya watu binafsi na biashara ndogo ndogo kwani hawa wakipata unafuu wataweza kukuza biashara zao na hivyo kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji.”

Akizungumzia suala la baadhi ya benki kuwa na  tawi moja au mawili jijini Dar es Salaam tu, Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuzitathimini upya benki za aina hiyo.

“Leo narudia tena kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuzisimamia benki zetu ili zifungue matawi yake hadi vijijini waliko wenye uhitaji.! Kwanini? benki nyingi zimejikita katika kutafuta faida pekee bila kuwekeza kwa faida ya nchi yetu? Hadi sasa tuna benki ambazo zimekuwa siku zote na tawi moja tu tena liko Dar-es-Salaam. Benki Kuu ya Tanzania isisite kuchukua hatua za kisheria kurekebisha hali hiyo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya TIB, Frank Nyabundege amesema kwa kipindi cha miaka minne benki hiyo imeweza kukuza mtaji kutoka Sh206 bilioni wakati inagawanywa mwaka 2015 mpaka kufikia sh. bilioni 409 mwishoni mwa mwaka 2018 sawa na ukuaji wa asilimia 98.5.

Mkurugenzi huyo amesema mbali na kufanikiwa katika kukuza mtaji, pia benki hiyo imeweza kukuza amana za wateja kutoka Sh110 bilioni mwaka 2015 mpaka Sh338 bilioni mwezi Disemba 2018, sawa na ukuaji wa asilimia 207.

Mafanikio mengine yabenki ya TIB katika kipindi cha miaka minne ni pamoja na kuanza kutengeza faida angalau ya Sh1.3 bilioni mwaka jana (2018), kutoa mchango stahiki katika Mfuko Mkuu wa Serikali kiasi cha Sh250 milioni.”

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa benki hiyo imetoa mikopo na dhamana kwa taasisi za umma hadi kufikia Sh224.35 bilioni kwa kipindi kilichoishia Machi 2019, kulipa kodi Serikalini kiasi cha Sh19.2 bilioni tangu benki ianzishwe na kutoa mikopo kwenye sekta ya viwanda jumla ya Sh65.12 bilioni.