VIDEO: Majaliwa kula sahani moja na wanaohujumu zao la chikichi

Muktasari:

  • Serikali yavalia njuga kilimo cha michikichi ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wakulima wa zao hilo wananufaika kama wakulima wa mazao mengine ya biashara.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali haitomvumilia mtu yeyote atakayebainika kuhujumu mkakati wake wa kulifufua zao la chikichi nchini.

Amesema wanataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama wengine wa mazao makuu ya biashara, hivyo haitomfumbia macho mtu atakayezembea.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Februari 18, 2019 na kitengo cha mawasiliano kwa ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa aliyasema hayo jana Jumapili mara baada ya kukagua shamba la michikichi la kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Bulombora.

Aliwaagiza viongozi mkoani Kigoma kuhakikisha kwamba suala la kilimo cha michikichi liwe ajenda ya kudumu kwenye vikao vyao.

Alisema Serikali inataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama ilivyokuwa kwa wakulima wa korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali imeamua kulifufua zao hilo ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula kwani inatumia fedha nyingi kuagiza nje ya nchi.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe shamba darasa la zao la michikichi ili wananchi waweze kujifunza mbinu bora za kulima zao hilo.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba alisema katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga zaidi ya Sh10 bilioni kwa ajili ya kuboresha kilimo cha zao hilo sambamba na kuongeza watafiti zaidi ya 10 wa zao hilo hilo katika Kituo cha Utafiti cha Kihinga.

Alisema iwapo kilimo cha zao hilo kitaboreshwa kitasaidia Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.