Maji ‘yatibu machungu’ ya wakazi wa Handeni

Thursday January 17 2019

 

By Raisa Said, Mwananchi [email protected]

Maji ni rasilimali muhimu katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwamo uchimbaji madini, uzalishaji viwandani pamoja na kilimo.

Hata hivyo, uvunaji wa rasilimali hii unahitaji uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu licha ya mabadiliko ya tabia nchi yanayotishia uendelevu wa vyanzo vilivyopo.

Wilayani Handeni mkoani Tanga juhudi zilizofanywa zimesaidia kuongeza uzalishaji sambamba na usambazaji wa maji, hivyo kupunguza kero iliyokuwapo kwa muda mrefu.

Kilio cha maji kwa wakazi wa Handeni kilikuwa kikisikika kila siku kutokana na kusababisha maisha kuwa magumu.

“Lilikuwa ni jambo ambalo linaninyima usingizi tangu nilipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili. Ulikuwa ni mtihani wa kuhakikisha waliompigia kura wanapata maji.

“Nilikuwa nikitafakari nitawezaje kumaliza tatizo ambalo watangulizi wangu walishindwa kulimaliza,” anasema mbunge huyo wa Handeni Mjini, Omari Kigoda.

Anasisitiza kuwa jambo ambalo limesaidia katika juhudi za kutatua kero hiyo ni ushirikiano mkubwa baina ya viongozi.

Aprili 2018, Mamlaka ya Maji Mjini Handeni ilipokea Sh277 milioni kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kuhuisha miundombinu ya maji Mjini Handeni.

Mbunge huyo anasema kwamba ushirikiano mkubwa baina ya viongozi umesaidia kufanikisha kupunguza kero ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Anasema wakati anachaguliwa mwaka 2015, wananchi waliokuwa wanapata majisafi walikuwa kati ya asilimia 25 na 30, lakini kwa sasa wameongezeka na kufikia asilimia 55 hadi 60.

Kwa kuthibitisha mabadiliko yaliyopo, Mwamisa Omari ambaye ni mkazi wa mjini Handeni anasema kero ya maji ilikuwa ‘inateteresha’ ndoa kutokana na wanawake wengi kulazimika kutafuta maji usiku jambo lililokuwa linawapa wasiwasi wanaume.

“Naomba nikueleze ukweli, ndoa yangu iliyumba sana mpaka kutaka kuvunjika kutokana na suala zima la maji,” anasema Mwamisa.

Mkazi wa Kwediyamba, Amina Omari anasema, walikuwa wananunua ndoo ya lita 20 kwa kati ya Sh500 mpaka Sh1,000; bei ambayo imeshuka mpaka Sh50.

INAENDELEA UK14

Anasema changamoto hiyo ilikuwa kubwa miaka ya nyuma lakini kuna kila dalili kuwa tatizo limeanza kupungua kwa kiasi kikubwa na kuwapa matumaini wakazi wote wa mji wa Handeni.

Mariamu Semdoe anaeleza kuwa ilifikia wakati alitamani hata kuhama katika mji huo wa Handeni kutokana na changamoto hiyo ya maji.

Mkazi mwingine, Ramadhan Khalidi anaeleza kuwa suala la maji lilikuwa ni changamoto kubwa na sugu iliyokuwa inafanya maisha yao kuwa magumu na kusababisha kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Asha Jumaa, mkazi wa kata ya Mdoe anasema kuanza kutoka maji katika kata yao limekuwa ni jambo la kufurahisha.

“Tangu dunia iumbwe sisi hatujawahi kupata maji kama ilivyo sasa,” anadai.

Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano pamoja mbunge wao kwa kuhakikisha wanaanza kupunguza tatizo hilo sugu la maji.

“Tumewahi kuwa na viongozi wengi lakini hawakuweza kupunguza changamoto hii licha ya kutupa ahadi ya kila mwaka. Kama wameweza kutatua tatizo hili kwa kweli tunaupongeza uongozi wa sasa umeweza kupunguza tatizo hili kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Licha ya umuhimu wake kwenye maisha ya binadamu na shughuli za maendeleo, upatikanaji wa majisafi na salama katika maeneo mengi nchini umekuwa na changamoto nyingi. Hata hivyo, ipo mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo.

Kaimu meneja wa Mamlaka ya Maji Handeni Mjini, Minja Charles anasema kwamba wamefanya ukarabati wa miundombinu ulioimarisha uzalishaji kutoka lita 158,000 hadi 514,000 kwa siku.

Vilevile, vituo 24 vya kuchotea maji vilivyopo barabara za Moto, Bomani, Mwanga, Kivesa, Chang’ombe na Vibaoni vimefufuliwa na vyote vinatoa maji.

Charles pia anasema kwamba vituo vipya vitano vimejengwa maeneo ya Azimio, Bomani na Seuta hivyo idadi ya vituo vinavyotoa maji kufikia 47 hadi sasa, huku wateja 129 ambao walikuwa hawapati maji wamerejeshewa huduma hiyo.

“Yamewezekana baada ya mamlaka ya maji Handeni Mjini kupokea Sh277.477 milioni kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kuhuisha miundombinu,” anasema Charles.

Naye mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe anasema kwamba wakati anaingia madarakani mwanzoni mwa mwaka 2016 alikuta vituo 52 havitoi maji lakini kutokana na juhudi walizofanya idadi hiyo imepungua.

“Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la uhaba wa maji Handeni ili wananchi wapate maji safi na salama,” anasema Gondwe.

Kwa upande wake, mhandisi wa maji wa halmashauri ya Mji wa Handeni, Dismas Kway anasema upatikanaji wa maji unaendelea kuimarika kwa kuwa wananchi wanayapata kwa wastani wa saa 15 kwa siku.

Hali hiyo anasema inatokana na kujengwa mradi mkubwa wa maji katika kata ya Malezi uliogharimu Sh518 milioni ukiwa na vituo 15 vinavyohudumia jumla ya wateja 3,750.

“Jumla ya wakazi 36,000 kati ya 84,000 waliopo Handeni Mjini wanapata maji safi na salama. Wananchi 48,000 waliobaki wanatumia visima vya asili,” anasema Kway.

Hivi karibuni wakati akitoa ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji kwa mwaka 2018, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mbarawa alisema: “Serikali imejipanga kuhakikisha mamlaka za maji zinajiendesha kibiashara kwa sababu zinaweza kujenga miundombinu mikubwa na ya kisasa.

“Kama mamlaka hazitofanya kazi hii kibiashara hatuwezi kuwafikia wananchi wengi.”

Kuhusu ankara za maji, anasema utozaji wa ankara usio na uwiano kwa wateja ni sababu nyingine ya ufinyu wa mapato kwa mamlaka za maji.

Anasema wapo wateja wanaokadiriwa ankara kubwa licha ya kutumia kiasi kidogo cha maji huku wanaotumia kiasi kikubwa hasa taasisi na makampuni mbalimbali wakilipa ankara ndogo hali inayoisababishia hasara kwa mamlaka za maji.

“Kwa mfano mimi napata maji natumia mita za ujazo 30 kwa mwezi, inatokea miezi miwili inaenda hiyo hiyo 30 lakini baadaye inaenda zinaenda hadi mita za ujazo 80, naona kuna changamoto pale,” anasema Waziri Mbarawa.


Advertisement