Maji ya mvua yafunga barabara eneo la Jangwani na Bonde la Mkwajuni Udart, yasitisha safari za mabasi yake

Dar es Salaam. Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), imesitisha huduma ya usafiri kwa muda leo Mei, 13 kwa mabasi yote yanayotumia barabara ya Morogoro eneo la Jangwani na Bonde la Mkwajuni kuelekea Morocco kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini hapa.

Eneo la Jangwani linafahamika kwa kujaa maji mengi barabarani kipindi cha mvua.

Taarifa ya Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Udart, Deus Bugaywa imeeleza kuwa safari zilizositishwa ni kati ya Kimara - Kivukoni,   Kimara - Gerezani, Morocco - Kivukoni na Morocco - Gerezani kuanzia saa 10: 30 alfajiri leo Jumatatu.

“Huduma zinazotolewa sasa ni kati ya Kimara - Mbezi, Kimara - Magomeni Mapipa, Gerezani - Muhimbili, Kivukoni - Muhimbili na Gerezani – Kivukoni” amesema Buyagwa.

Udart wameomba radhi na kueleza kuwa wanaendelea kufuatilia hali ya maji Jangwani na yakipungua huduma zitaendelea kutolewa.