VIDEO: Majirani wamlilia mwanamke anayedaiwa kuuawa na mumewe

Muktasari:

Simanzi imetawala kwa wakazi wa mtaa wa Geza juu Kigamboni jijini Dar es Salaam alikokuwa akiishi, Naomi Marijani anayedaiwa kuuawa na mumewe, Khamis Luwonga kutokana na majirani zake kudai alikuwa kinara wa kuhamasisha wanawake kujikita katika biashara

Dar es Salaam. Simanzi imetawala kwa wakazi wa mtaa wa Geza juu Kigamboni jijini Dar es Salaam alikokuwa akiishi, Naomi Marijani anayedaiwa kuuawa na mumewe, Khamis Luwonga kutokana na majirani zake kudai alikuwa kinara wa kuhamasisha wanawake kujikita katika biashara.

Wametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 17, 2019 wakati wakizungumza na Mwananchi lililofika nyumba aliyokuwa akiishi Naomi na kukuta imezungushiwa utepe wa Polisi.

Mmoja wa majirani hao, Sabina Manyanda amesema taarifa za kifo zimewashtua na kuwaachia simanzi hasa wanawake.

“Alikuwa mcheshi na mwenye upendo habari za kupotea kwake tulizisikia tukawa tunashindwa kuelewa inakuwaje mtu mzima apotee.”

“Jana ndiyo wamekuja askari na ndio tukasikia  amekutwa na matatizo hayo, kwa kweli ni pigo kwetu alikuwa mhamasishaji mkubwa wa wanawake kufanya biashara,” amesema Manyanda.

Neema John amesema taarifa ya kifo cha Naomi imemshtua kwa kuwa hawakuwahi kama alikuwa na matatizo na mumewe kiasi cha kufikia hali hiyo.

“Nashindwa kueleza ni namna gani nimeguswa na taarifa hii, huyu dada ni jirani hapa na tulikuwa tukiishi vizuri, muda wote anafurahi sikujua kwamba ana matatizo,” amesema Neema huku akishindwa kuzuia machozi kutoka.