Majokofu 1,385 ya kutunzia chanjo kusambazwa vituo vya afya

Muktasari:

  • Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na shirika la Gavi imenunua majokofu 1,385 kwa ajili ya utunzaji wa chanjo katika vituo mbalimbali na vishikwambi 1,249 kwa ajili ya kukusanya taarifa za chanjo kwa njia ya mtandao badala ya makaratasi.

Dar es Salaam. Majokofu 1,385 ya kutunzia chanjo yenye thamani ya Sh13.9 bilioni yanatarajiwa kusambazwa katika vituo mbalimbali vya afya na hospitali nchini.

Mbali na majokofu hayo pia Serikali imetambulisha mfumo mpya wa ukusanyaji taarifa za chanjo kwa njia ya mtandao, kupitia vishikwambi (tablet)

Akizungumza leo Ijumaa Februari 22, 2019, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema majokofu na vishikwambi kwa pamoja vitasaidia kuimarisha huduma za chanjo nchini.

“Kuna majokofu ya aina mbili, yale yanayotumia nishati ya jua 1,190 na yanayotumia umeme 195. Yote yana thamani ya Sh13.9 bilioni ambapo jokofu linalotumia nishati ya jua ni Sh10 milioni na lile la umeme limegharimu Sh5.3 milioni,” amesema Waziri Ummy.

Amesema gharama iliyotumika kununua vishkwambi vyote ni Sh1.5 bilioni ambapo kila kimoja kina thamani ya Sh1.2 milioni.

Waziri Ummy amesema vishkwambi na majokofu hayo yaliyopokelewa leo ni awamu ya kwanza kwani wanatarajia kupokea kati ya 800 hadi ,1000 na vishkwambi zaidi ya 3,000 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

“Majokofu yatafungwa katika vituo vipya vya afya na baadhi vile vya zamani lakini pia tutapeleka katika mikoa 15 na awamu ya pili tutafanya mikoa mingine iliyobaki,” amesema.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Bakari Kambi, amesema kimataifa Tanzania imefanya vizuri katika chanjo kwa mwaka 2016/17.

“Asilimia 97 ya watoto tuliweza kuwachanja lakini lengo letu ni kufikia asilimia 100. Kuletwa kwa majokofu haya ni kuhakikisha mnyororo wa chanjo unakaa vizuri na ni namna wizara inafanya kazi nzuri na wadau mbalimbali,” amesema Profesa Kambi.