Makada CCM waonywa kura za misikitini, makanisani

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi, kimewaonya makada wa chama hicho,wenye nia ya kugombea ubunge, kuacha kujipitisha makanisani na misikitini kuomba kura, kwa kuwa chama hicho hakijatangaza uchaguzi wa wabunge.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk Bashiru Ally, amewaonya makada wa chama hicho, wenye nia ya kugombea ubunge, kuacha kujipitisha kwenye nyumba za Ibada kuomba kura.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Julai 8, 2019,wakati akizungumza na viongozi wa chama na Serikali wa wilaya ya Moshi Vijijini ambapo amesema makanisani na misikitini ni maeneo ya kwenda kuchoma dhambi na si kuomba kura.

"Chama hakijatangaza uchaguzi wa wabunge, wale wanaotaka kugombea, acheni tabia za kwenda misikitini na makanisani kutafuta kura, huko mnatakiwa kwenda kuchoma dhambi zenu," amesema Dk Bashiru.

"Nasikia kuna baadhi ya wagombea wamekuwa wakarimu kuliko wakati wote, kwenye misiba wapo, kwenye mahafali wapo kipaimara wapo, halafu wanaanza kutangaza sahani hizi zimeletwa na fulani, jamvi hili limeletwa na fulani, wacha kujipendekeza."

"Fanyeni kazi na sisi tutawahakiki kazi zenu,” alisema na kuongeza, “halafu siasa hizo unazifanya Kilimanjaro, utafanya utajipendekeza lakini wao wanajua, watakupiga chini."

Amesema upande wa chama wako vizuri na upande wa wagombea nako wawe vizuri, na kupeleka watu ambao wananchi wakiwaona watasena huyu ni mgombea wa CCM, anakwenda kutenda na kuwatumikia wananchi.

Ametumia pia nafasi hiyo, kuwaonya watendaji na viongozi wa chama, kuepuka kuwabeba wagombea na kuhakikisha wanatenda haki.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema kazi kubwa waliyonayo sasa ni kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.