Makamba: Hatujashtukiza kuzuia mifuko ya plastiki

Muktasari:

  • Serikali imesema kuwa uamuzi wake wa kupiga marufuku matumizi ya  mifuko ya plastiki nchini si wa kushtukiza bali ni mpango wa muda mrefu.

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba amesema uamuzi wa Serikali wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki siyo wa kushtukiza bali ni mpango wa muda mrefu.

Hata hivyo, amesema siyo mifuko yote ya plastiki itakayozuiliwa matumizi yake, bali kuna baadhi ya vifungashio vya plastiki vitaendelea kutumika kama vile vya dawa za binadamu, pembejeo za kilimo, vya kiwandani, vya ujenzi na vya maziwa.

Amesema marufuku itakuwa ni kwa mifuko ya plastiki ambayo mara nyingi ndiyo inayolalamikiwa kuchafua mazingira duniani.

“Kuna watu watasema kuwa tukipiga marufuku mifuko hiyo tutapoteza ajira kwa wananchi na kuua viwanda vyetu, hapana maana asilimia 80 ya mifuko hiyo haitengenezwi hapa nchini inatoka nje ya nchi na kuletwa hapa nchini kwa ajili ya matumizi kwa hiyo kama ni kuuwa viwanda basi tutauwa viwanda vya nje ya nchi na siyo vya hapa nyumbani.”

“Tumejipanga vizuri kwa ajili kuanza kutumia mifuko mbadala ya plastiki hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kupigwa marufuku mifuko ya plastiki nchini ndiyo itakuwa mwisho wa maisha, hapana, matumizi ya mifuko ya plastiki yameanza takribani miaka 15 tu nyuma kabla ya hapo haikuwepo,” amesema Makamba.

Aidha, amesema kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakiipigia kelele mifuko hiyo kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira, hivyo Serikali imeamua kuipiga marufuku na kuanza kutumia mifuko mbadala.

Amesema katika marufuku hiyo wamewashirikisha wadau wote wakiwamo wananchi, watengenezaji wa mifuko hiyo, wasambazaji na waagizaji na kupata maoni yao ambapo katika barua yao kwa waziri huyo shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI) waliitaka Serikali kuweka marufuku hiyo tangu Disemba 31, 2017.

Amesema kilichobaki kwa sasa ni Serikali kuandika kanuni za katazo la kisheria kwenye gazeti la Serikali, kutoa elimu kwa umma, kufafanua ni vifungashio gani vya plastiki ambavyo havijapigwa marufuku na namna ya kuvikusanya baada ya matumizi.

“Pia Serikali itaweka kikosi kazi maalum cha kusimamia katazo hilo kutoka katika mamlaka mbalimbali za kiserikali ikiwamo, NEMC, TFDA, TBS, TRA na wizara ya mambo ya ndani ya nchi ambao watafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kusimamia katazo hilo ambapo adhabu mbalimbali zitatolewa kwa watakaokaidi,” amesema Makamba.

Mapema jana bungeni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini ni Mei 31 mwaka huu na kuwataka wenye viwanda vinavyozalisha mifuko hiyo kubadilisha teknolojia na viwanda vyao.