Makamba: Mengi alikuwa nembo ya Tanzania duniani

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia leo alikuwa ni nembo ya Tanzania duniani

 

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo alikuwa ni nembo ya Tanzania duniani.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 2, Makamba amesema Mengi alikuwa na mchango mkubwa  katika tasnia ya habari, biashara na mazingira.

Amesema pia alihamasisha vijana kufanikiwa katika biashara wakati wa uhai wake.

Makamba amesema kifo cha Mengi ni pigo kwa taifa katika biashara na habari.

“Ni nembo ya Tanzania duniani kwa sababu alikuwa akitajwa katika majarida mbalimbali, pembeni mwa jina lake inatajwa Tanzania,  alikuwa balozi wa Tanzania,” amesema Makamba.

Amesema Mengi atakumbukwa pia kwa kitabu chake alichokiandika ambacho kimetoa hamasa kwa vijana katika biashara.

“Kila harambee kubwa ya kijamii pia Mengi alishiriki na kuchanga, hakuwa mfanyabiashara tu bali alikuwa mwanajamii kwa hiyo tutamkumbuka kwa hilo.

Ameacha alama kubwa sana katika nchi yetu,” amesema.

Pia Makamba amesema kuwa Mengi atakumbukwa kama mtu wa kwanza aliyeanzisha kituo cha televisheni cha binafsi Tanzania Bara.