Makamba: Tumefanikiwa mifuko ya plastiki asilimia 100, bado bei - VIDEO

Dar es Salaam. Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Serikali ilipopiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ameeleza jinsi walivyoiondoa sokoni kwa karibu asilimia 100.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi jijini Dar es Salaam juzi, Waziri Makamba alisema vita hiyo ilifanikiwa kwa kuwa ilihusisha watendaji wa Serikali na wadau wengine.

“Asilimia karibu 100 ya wananchi waliokuwa wakitumia mifuko hiyo sasa wanatumia mifuko mbadala, ukienda kila pahala, kila soko, kila genge kwa asilimia 99.9 huwezi kukuta mifuko ya plastiki. Kwa hiyo sisi kwa tathmini yetu tumefanikiwa tulichotaka kukifanya,” alisema Makamba.

Alisema katika operesheni hiyo kulikuwa na mfululizo wa vikao vya kimkakati mchana hadi usiku, “kama wiki mbili tatu kabla ya tarehe moja (Juni Mosi) kulikuwa na mikanganyiko mingi, tulikuwa tunawasiliana haraka sana. Airport wafanyeje, wanaoingia mipakani, namba za simu wanaotaka taarifa zaidi na mambo mengine,” alisema.

Alisema siku ya utekelezaji kulikuwa na hofu ya kutokea vurugu na mkanganyiko ikiwa pamoja na nguvu kubwa kutumika na kusababisha kero kwa wananchi, “Kulikuwa na maombi ya kuahirisha, kwamba hatuko tayari. Kwa sababu tulishaweka msimamo tukabaki na msimamo huohuo.

“Kulikuwa na njama za hujuma pia, ili ionekane tarehe moja ionekane imefeli tuahirishe. Lakini tukaendelea na tukafanikiwa vizuri.”

Kuhusu gharama za mifuko mbadala, Makamba alisema bei yake ambayo ipo juu kwa sasa itashuka siku za usoni baada ya kuingizwa kwa mitambo ya kutengeneza mifuko iliyoagizwa nje ya nchi ifikapo Septemba.

“Bahati mbaya mipango ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki ilikuwa ikiahirishwa. Watengenezaji wa mifuko walipojitokeza kuingiza mitambo ya kutengeneza mifuko mbadala tuliahirisha.

“Kutokana na hiyo, mifuko mbadala na mitambo ya kuzalisha ikachelewa kuingia. Kuna wanaotuambia wana mitambo na mifuko kwenye meli. Tunaamini itakapofika Septemba mifuko mizuri itakuwepo kwenye soko,” alisema.

Baada ya kufanikiwa kwenye chupa, Waziri Makamba alitangaza katazo jingine ni la matumizi ya chupa za vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) vinavyozalishwa nchini ili kulinda mazingira.

Hata hivyo, alisema katazo la chupa hizo nyeusi halitakuwa operesheni kama zilivyo nyingine, bali ameshazungumza na kampuni zinazotengeneza vinywaji hivyo, “ukienda mtaani utakuta kuna vijana wanabeba chupa za plastiki, changamoto ni chupa za ‘energy drinks’ hizi nyeusi. Ukienda kwenye mifereji mingi kwenye mito utazikuta.”

Alisema kuzagaa kwa chupa hizo kunasababishwa na bei ndogo na hivyo kutowavutia waokotaji, “zile nyeupe ni Sh400 kwa kilo, zile nyeusi Sh80 au 100.

“Tumeongea na wazalishaji wa chupa nyeusi ambao wakubwa ni wawili, Azam na Mohamed Enterprises, tumekubaliana kuwa watabadilisha mfumo wenyewe ili chupa zisiwepo na wamekubali. Itafika mahali hazitakuwapo tena.”