Makamba apigia msumari zuio usafirishaji taka hatarishi

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba jana amepigilia msumari wa zuio la usafirishaji wa taka hatarishi huku akieleza sababu zilizochagiza uamuzi huo

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira , January Makamba jana amepigilia msumari wa zuio la usafirishaji wa taka hatarishi nje ya nchi huku akieleza sababu zilizochagiza uamuzi huo.

Machi 22, 2019 Waziri Makamba aliweka zuio la wiki tatu la usafirishaji wa chuma chakavu na taka hatarishi kwenda nje ya nchi hadi utakapofanyika uhakiki wa vibali vilivyotolewa na mamlaka mbalimbali kwa ajili ya kuweka utaratibu wa udhibiti.

“Bado zuio hilo limebaki kutoa nje na kuingiza kwa sababu tunahitaji uhakika wa kinachotoka na kuweka mifumo itakayotuhakikishia kile kinachotoka nje kitolewe kwa utaratibu wa sheria za nchi na mikataba ya kimataifa tuliyosaini,” alisema Waziri Makamba jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na wadau takriban 300 wanaohusika na biashara ya taka hatarishi nchini.

 

“Kwa mfano mkataba wa kimataifa unaeleza hauwezi kupeleka taka kwenye nchi nyingine kabla ya nchi hiyo haijtoa ridhaa ya kupokea. Kwa hiyo hata Tanzania tukitoa kibali cha kusafirisha bila kuona ridhaa ya nchi kupokea, tutakuwa tumevunja wajibu wetu kwa hiyo tumesimamisha ili kuweka mifumo kutimiza wajibu wetu kimataifa,” amesema.

 

Mkutano huo ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ulikutanisha wadau kutoka kampuni 27 zinazohusisha wakusanyaji, wanunuzi, wauzaji, waingizaji na wasafirishaji wa taka hatarishi nje ya nchi. 

Baadhi ya taka hizo ni pamoja na zile zinazozalishwa hospitalini, migodini, mafuta machafu, vyuma chakavu na taka za kielektroniki.

Waziri Makamba amesema kati ya Januari hadi Machi mwaka huu, makontena 280 za vyuma chakavu yalisafirishwa nje kwa njia rasmi ya Bandari ya Dar es Salaam huku nyingine zikisafirishwa kwa njia za uchochoro kuingia mipaka ya nchi jirani, ambazo zingeweza kuwa malighafi ya uzalishaji, ajira na kipato nchini.  

“Sababu nyingine ya kuzuia ilikuwa ni kujihakikishia kinachoingia na kutoka,tulibaini kwamba wakati mwingine yaliyosemwa yanaondoka, kumbe siyo yenyewe yaliyoondoka (makontena ya taka),” amesema.

Waziri Makamba ametaja sababu nyingine ni kulinda malighafi kwa viwanda vikiwamo vinavyotengeneza nondo na mwisho ni tahadhari ya nchi kupokea taka, akisema hakuna utayari huo.

Katika mkautano huo, Serikali na wadau hao wamekubaliana kuweka mfumo utaoongeza idadi ya taasisi zinazotoa vibali, kuongeza ufuatiliaji wa kisheria chini ya NEMC, udhibiti wa vibali kwa waombaji.

Mwakilishi wa kampuni ya Focus Environmental inayojihusisha na biashara ya vyuma chakavu na taka hatarishi, Athman Hamis amesema mkutano huo umekuwa na tija maeneo matatu ambayo ni hoja za utengenezaji wa fursa za ajira, usimamizi katika maombi ya vibali na kupunguza urasimu kwa taasisi za Serikali.

“Kwa upande wangu mkutano ulikuwa mzuri na umekuwa na matumaini ya kuimarisha shughuli hizi, kinachotakiwa ni utekelezaji, kwa mfano eneo la urekebishaji tozo za vibali vya vyuma chakavu, zirekebishwe kwenye kanuni ni nyingi sana Sh10 milioni,” amesema mdau mwingine wa mazingira, Raymond Thomas.