Makamba asema mwongozo wa mifuko mbadala utawasaidia Watanzania

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira), January Makamba wa pili kulia akiangalia mfuko mbadala uliotengenezwa na kiwanda cha Green Earth Papers Product alipotelembelea leo.

Muktasari:

  • Makamba asema mwongozo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) utarahisisha Watanzania kutofautisha mifuko mbadala ya kubebea nyama na bidhaa nyingine.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema mwongozo wa ubora kuhusu sifa za mifuko mbadala utasaidia Watanzania kujua mifuko itakayotakiwa kuwekewa  nyama na utumbo au bidhaa nyingine.

Amesema si kweli hakuna mifuko mbadala haina sifa za kubebea nyama au utumbo, mifuko hiyo ipo lakini wananchi wanashindwa kuitofautisha

Makamba ameeleza hayo leo, Jumatatu Juni 3, 2019 wakati wa ziara ya kutembelea viwanda vya kuzalisha mifuko mbadala kikiwemo cha  Green Earth  Paper Product kilichopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

"Hatua ya ubora utakaowekwa na TBS (Shirika la Viwango Tanzania) utasaidia wananchi kuijua vyema mifuko hii mbadala kwa sababu itakuwa na nembo maalumu. Wengi hawajui kuitofautisha mifuko hii, naomba tusiseme kuwa hakuna mifuko mbadala ya kubebea nyama au utumbo," amesema Makamba.

Makamba ametumia nafasi kukipongeza kiwanda hicho, ambacho kinatengeneza mifuko mbadala ambayo inayochukuliwa na taasisi za Serikali na wadau mbalimbali yakiwemo maduka makubwa.

Mkurugenzi wa Green Earth Papers Paper Product, Sebastian Seraphin amesema wanazalisha mifuko mbadala  ya matumizi ya kawaida kuanzia kilo moja na kuendelea  na ile inayotumika na maduka makubwa

"Kwa sasa tunazalisha tani 1 na nusu, tuna wafanyakazi 20, ambao kila mmoja anatengeneza mifuko 400 kwa siku," amesema Seraphin

 

 

Seraphin ameishukuru Serikali kwa kupiga marufuku mifuko hiyo akisema hivi sasa wanapata oda nyingi tofauti na siku nyuma wakati mifuko ya plastiki ikiendelea kutumika.

"Sasa hivi tuna oda ya tani 15, kutoka kwa wafanyabiashara, taasisi za Serikali na watu wa kawaida. Tunajitahidi ndani ya siku tano tuzikamilishe ili tuwapelekee mizigo yao.”

"Miezi mitatu ya awali tulikuwa tunapokea oda za Sh20 milioni hadi Sh30 milioni kwa mwezi, lakini wiki tatu au nne kabla ya katazo kuanza kutumika Juni Mosi tumepokea oda za zaidi ya S 100 milioni. Kiwango cha mifuko mbadala kimeongezeka sasa hivi tunazalisha mifuko zaidi ya 100,O00 kwa siku, " amesema Seraphin.