Makamba atangaza fursa kwa wazalishaji wa nishati mbadala

Muktasari:

Serikali ipo tayari kuwasaidia vijana wanaokuja na wazo la kutafuta nishati mbadala ya kupikia mbali na mkaa na kuni.


Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za wajasiriamali wanaovumbua nishati mbadala.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Februari, 2019 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Januari Makamba alipokuwa akizungumza kwenye mdahalo wa Mwananchi Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na ITV Redio One.

Makamba amesema anafarijika anapoona kuna vijana wanaotafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

"Nilikwenda mkoani Tabora nikakuta vijana wanapambana na wamekuja na wazo la kuzalisha mkaa mbadala, nikashirikiana na wadau kuwawezesha na nitafanya hivyo kwa yeyote atakayeonyesha nia ya kufanya hivyo," amesema Makamba.