Makamba azungumzia tena kutenguliwa kwake

Muktasari:

Makamba atoa neno la kumshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini, makamu wa rais, waziri mkuu na mawaziri wote, awapongeza Bashe na Simbachawene awaahidi kuwapa ushirikiano wa dhati.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kumwamini katika nafasi hiyo.

Makamba ameandika ujumbe huo leo Jumatatu Julia 22, 2019 kupitia akaunti yake Twitter ikiwa ni saa chache baada ya Rais Magufuli kuwaapisha mawaziri George Simbachawene aliyechukua nafasi yake (Makamba) na Hussein Bashe anayekwenda kuwa Naibu Waziri wa Kilimo akichukua nafasi ya Innocent Bashungwa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Jana Jumapili, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wa Makamba na kumrejesha tena Simbachawene aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), miaka miwili iliyopita.

Katika ujumbe huo, Makamba ameandika, “Neno la mwisho kwenye hili: Namshukuru Rais kwa kuniamini, Makamu wa Rais kwa kunielekeza, PM (waziri mkuu) kwa kunisimamia, na Team ya VPO(ofisi ya makamu wa rais)/NEMC na mawaziri wote kwa ushirikiano.”

“Nampongeza @HusseinBashe na Simbachawene kwa kuaminiwa. Nawatakia heri na kuwaahidi ushirikiano wangu wa dhati,” ameongeza Mbunge huyo wa Bumbuli.

Ujumbe wa kwanza kuutoa Makamba baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake, aliandika katika akaunti zake za kijamii akisema, “Kwa kweli nimeyapokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa kabisa. Nitasema zaidi siku zijazo.”

Ujumbe huo wa Makamba aliuambatanisha na picha aliyokaa pamoja na Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi wakiwa wenye furaha.