Makamba azungumzia utaratibu wazalishaji kuondoa chupa za plastiki zilizotumika

Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba 

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema Serikali ya Tanzania itaweka utaratibu utakaowalazimu waingizaji na wazalishaji wa  chupa za plastiki nchini kuziondoa kwenye mazingira.


Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema Serikali ya Tanzania itaweka utaratibu utakaowalazimu waingizaji na wazalishaji wa  chupa za plastiki nchini kuziondoa kwenye mazingira.

Makamba ameeleza hayo leo Jumamosi  Julai 20, 2019 alipotembelea kiwanda cha Paper Craft International kinachomilikiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa Group kinachozalisha  vifungashio vya karatasi.

Amesema  Serikali haijapiga  marufuku chupa za plastiki kwa sababu zina uwezo wa kurejelezwa, baadhi zikiwemo zinazozalishwa na Azam zimekuwa hazina soko na watu hawazikusanyi na kuondolewa kwenye mazingira.

“Ukienda kwenye mifereji na fukwe utakutana na chupa nyingi  ambazo hazikusanywi kwa sababu hazina soko na miezi ijayo tutaweka utaratibu wa kuwalazimisha kuziondoa chupa hizi kwenye mazingira.”

“Ingawa tunafanya mambo mazuri kwenye mifuko na mazingira, lakini chupa za plastiki zina madhara katika mazingira,” amesema Makamba.

Kuhusu kiwanda hicho, Makamba amesema endapo kitaanza kuzalisha vifungashio hivyo kwa ajili ya soko la ndani itarahisisha upatikanaji mkubwa wa bidhaa hiyo, hasa baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni mosi, 2019.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa kiwanda hicho , Hussein Sufian amesema  wameshaanza mazungumzo ya ushirikiano wa namna ya  kuandaa mchakato wa ukusanyaji wa chupa ili zitengeneze bidhaa mbadala.