Makonda aeleza jinsi marais 16 wa SADC watakavyopokelewa Tanzania

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

  • Katika kuelekea mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) Agosti 2019, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema wanajipanga kuhakikisha marais 16 watakaoshiriki mkutano

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema amejipanga kuhamasisha wananchi kujipanga kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mpaka Ikulu ya Tanzania kwa ajili ya kuwapokea marais 16 watakaoshiriki mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc).

Mkutano huo wa SADC utafanyika  Agosti 17  na 18 mwaka 2019 ambapo Rais wa Tanzania, John Magufuli atakuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao mara ya mwisho ulifanyika nchini humo mwaka 2003 na kuongozwa na Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa.

Akizungumza leo Jumanne Juni 25, 2019 katika uzinduzi wa taifa Gesi unaofanywa na Rais Magufuli Kigamboni jijini Dar es Salaam, Makonda amesema kama mkoa umepata heshima ya kujiandaa kupokea marais 16 kutoka nchi mbalimbali ndani ya Afrika.

“Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wa Dar es Salaam kuwa tuhakikishe shamrashamra zetu, tumekubaliana Simba na Yanga tunaacha tofauti zetu na tunajipanga uwanja wa ndege hadi Magogoni (Ikulu) kuwaonyesha hao marais wanaokuja kuwa wewe ndiyo mfalme wa taifa letu la Tanzania,” amesema Makonda.

Juni 12 mwaka 2019  Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza na wamiliki na wakuu wa vyombo vya habari nchini humo kuhusu mkutano huo alisema zaidi ya wageni 1,000 watakuwa katika Jiji la Dar es Salaam hivyo kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo. 

 

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gesi,  Khamis Ramadhani akizungumzia  uzinduzi huo alisema wameongeza uwezo wa kuhifadhi gesi katika ghala la Kigamboni kutoka tani za ujazo 1,650 hadi tani za ujazo 7,650 kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2018.

Mbali na uwezo huo pia imefanikiwa kuhifadhi kwenye maghala na mitambo ya gesi katika mikoa 20

Amesema uwekezaji huo umeifanya kampuni kuongoza katika idadi ya mitambo ya gesi pamoja ghala la mitambo mikubwa katika nchi za Afrika ya Mashariki na kusini mwa Afrika.

“Uwekezaji wote huu umegharimu takribani Sh150 bilioni na tunajivunia kufikia hatua hii.”

“Tumetekeleza mradi huu mkubwa kwa mara moja kwa sababu nchi yetu ina watu milioni 55, kama kila familia ina watu watano tuna familia 11, kila familia ikitumia kilo 15 za gesi kwa mwezi mahitaji yatakuwa tani 165,000 ikiwa ni sawa na tani milioni 2 kwa mwaka,” amesema

“Kama asilimia 30 ya Watanzania watatumia gesi basi tutakuwa na mahitaji ya tani 600,000 kwa mwaka hii ni sawa na kilo 11 kwa kila mtu kwa mwaka,” amesema Ramadhani.