Makonda amvaa Lissu kuhusu Mbowe, ajibiwa

Monday January 21 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema Tundu Lissu ndiye alihusika kuwashawishi mawakili kujitoa katika kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili aendelee kuteseka.

Amesema Lissu alifanya hivyo ili apate nafasi ya kusaka urais.

Hata hivyo, Lissu amekana akisema Makonda anatafuta ‘huruma’ ambayo hawezi kuipata.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Makonda aliandika Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alifanya hivyo kwa kutumia nafasi yake ya urais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Makonda aliandika ujumbe huo akiambatanisha na picha iliyomwonyesha Mbowe pamoja na mbunge wa Tarime Mjini kupitia chama hicho, Esther Matiko wakiwa Mahakamani Kuu.

Hata hivyo, Lissu amekana madai hayo akisema, “Makonda anapaswa kuwa mtu wa mwisho kuniambia chochote juu ya mwenyekiti wangu wa chama, kwa sababu Mbowe yupo gerezani kwa unyanyasaji wa Serikali ambayo Makonda ni sehemu yake.”

Kuhusu ziara aliyofanya Uingereza hivi karibuni, Lissu alisema, “Ziara hizo zinamsaidia sana Mbowe kwa kuieleza dunia kuwa Tanzania tumefikia mahali Serikali inamweka ndani kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani kwa sababu za kisiasa.”

“Nitawaeleza, nitawaeleza na nitaendelea kuwaeleza juu ya ukandamizaji unaofanywa kwa wapinzani. Kwa hiyo huyo anayesema nimemtelekeza Mbowe mwambieni namsaidia sana sana na asitafute huruma kwa jambo ambalo kila mtu analiona.”

Katika andiko lake, Makonda alisema alitegemea kumuona Lissu kama mwanasheria akiwa tayari amerejea nchini kumsaidia Mbowe, lakini kutokana na alichodai uroho wa madaraka anatumia matatizo ya mwenyekiti wake kujiimarisha kisiasa na kusaka urais.

“Hauhangaiki wala hata haufikirii kwamba ni wakati muafaka kurudi kuja kumpa moyo kama ambavyo alifanya yeye. Kweli hayo ndio malipo unayompa Mbowe kwa kukuhangaikia wewe upate matibabu bora,” aliandika Makonda.

Alisema wakati Lissu alipopata matatizo Mbowe ndiye alimpigania kutafuta fedha, kukaa naye Nairobi na kwenda hadi Ubelgiji, lakini kwa sasa ameamua kumuacha ateseke.

“Namalizia kwa kushangaa, leo watu waliochukua madini yetu, waliotutawala na kuwafanya watu weusi kuwa watumwa leo unawaomba wakuunge mkono ili uwe Rais.”

Makonda alisema, “Utakuwa Rais wetu au wa watu weupe, tutakuwa tumekuchangua sisi au umechaguliwa na Wazungu. Hivi unapitishwa na Wazungu kugombea urais au na wanachama wa chama chako, ni vikao vingapi vya chama haujahudhuria.”

Alisema ziara anazofanya Lissu hazina tija yoyote isipokuwa zinaichafua Serikali na nchi, na yeye (Lissu) akiwemo.


Advertisement