Makonda asimulia mama yake alivyonyang'anywa samani za nyumba

Muktasari:

  • Tuzo za Malkia wa Nguvu zinazoandaliwa na Clouds Media Group zimetolewa Dar es Salaam ambapo mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda ametumia fursa hiyo kuelezea jinsi mama yake alivyojitoa kuhakikisha anasoma

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mama yake alinyang’anywa samani za ndani baada ya kushindwa kulipa deni alilokopa taasisi ya fedha kwa ajili ya kumsomesha.

Makonda amesema hayo leo Jumamosi Aprili 6, 2019  kwenye utoaji wa tuzo za Malkia wa Nguvu zinazofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Amesema kila akifikiria tukio hilo anaamini wakina mama wanafanya kazi kubwa sana kwani mama yake alikuwa radhi adaiwe ili yeye asome na leo matunda yake yanaonekana.

Kutokana na hilo, amesema mama yake alifilisika na kulazimika kwenda kuuza samaki wanaoitwa mapanki eneo la Igoma jijini Mwanza na kumsomesha hadi kumaliza.

"Leo hii najivunia mama yangu kwani ndiye amesababisha leo nimekuwa mkuu wa mkoa kwa kujinyima kwake mimi nisome kwani kama angekata tamaa sijui leo ningekuwa wapi," amesema Makonda.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwashauri wasichana kubadili mfumo wao wa maisha  na kuhakikisha wanafanya jambo ambalo wataacha alama hata kesho wakiwa hawapo duniani badala ya kuishi maisha ya 'kick'.

Kutokana na ushuhuda huo aliyewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika, Gertrude Mongela amesema alichokisema Makonda ni ushahidi kwamba wakina mama hawana tatizo lolote.

Mongela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema wanawake wana nguvu kubwa na ana imani siku wakifutwa Tanzania wanaume watakufa.

Mama huyo ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa Ukerewe, amesema wanawake walioshinda tuzo hizo leo wana kila sababu ya kuonyesha nguvu yao kwa jamii.

"Tunataka kupitia nyie mliopata tuzo leo miaka 10 ijayo mtuzalishie malkia wengine na muonyeshe kwamba sisi ni jeshi kubwa," amesema Mongela.

Baadhi ya wanawake waliopewa tuzo akiwemo Marian Said, ambaye ni muuza vichwa na miguu ya kuku, aliwashauri wakina mama kutokata tamaa na kuwa wabunifu katika biashara zao.

Wakati Roby Samuel, anayemiliki kituo cha kulea watoto wanaokimbia vitendo vya ukeketaji mkoani Mara amesema hakujua kama siku moja kazi za wakina mama wanazozifanya vijijini zitaonekana na kuwashukuru Clouds kwa kuandaa tuzo hizo ambazo amesema zitaleta chachu kwa wanawake kujituma katika sekta mbalimbali.

Mwanasaikolojia maarufu, Sadaka Gandi, amesema Clouds wamekuwa moja ya kampuni inayowashika mikono wanawake wengi, kwani ndio waliomtoa kwa mara ya kwanza wakati anatoa elimu ya saikolojia ambayo awali ameeleza ilikuwa ikichukuliwa kama ni masuala ya matatizo ya akili.

"Anashukuru leo jamii imewaelewa wanasaikolojia ni kina nani na wengi wanaopata matatizo hukuta wakieletwa kwetu kwa ajili ya kupatiwa ushauri na tunashukuru tumeokoa wengi wakiwemo wanandoa," amesema Sadaka maarufu kwa jina la Auntie Sadaka.

Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga ameshukuru namna watu walivyojitokeza na kuwahakikishia kwamba wataendelea kuboresha tuzo hizo kila wakati.