Makonda ataka Watanzania wamsamehe Lissu, amtaka Spika Ndugai...

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa, Paul Makonda amezungumzia mahojiano aliyofanyiwa Tundu Lissu katika kipindi cha Hard Talk akitaka Watanzania wamsamehe lakini akimwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kumpeleka milembe atakaporejea nchini

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kumpeleka Tundu Lissu Hospitali ya Milembe baada ya kurejea nchini akitokea nchini Ubelgiji.

Makonda ameyasema hayo leo Jumanne Januari 22, 2019 katika mkutano wa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli.

Makonda amesema Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), katika mahojiano aliyoyafanya na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwenye kipindi cha Hard Talk nchini Uingereza alikuwa akijibu kama siyo Mtanzania kutokana na ‘kubwabwaja’ kwake huku mtangazaji akionekana kuwa mzalendo kuliko yeye.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa ni kuhusu juhudi za Rais Magufuli katika sekta ya madini namna anavyopambana kuhakikisha kodi zinalipwa, ila katika majibu yake alibadilika na kuanza kuzungumzia kuwa malipo yanaendelea.

“Lakini moja ya kitu nilichokuja kugundua kuwa tuna haki ya kumsamehe na Watanzania wote ni mwishoni alisema yeye bado mgonjwa hivyo naona kichwani mambo hayajakaa vizuri ndiyo maana anahitaji matibabu na akitoka kule basi Spika amfikishie Milembe, kule aendelee kutibiwa,” amesema Makonda.

Pia, Makonda alitumia muda huo kumtaka Rais Magufuli kusimama imara kila anachokifanya ili kuhakikisha hakuna kitu kinachomtikisa kwa sababu jukumu la kuongoza nchi amekabidhiwa yeye na Mungu.

“Usihangaike na watu ambao wamekataa kukuunga mkono, bali endelea kuungana na wale wanaosimama na wewe katika kila kitu,” amesema Makonda.