Makonda atoa siku saba Ma DC kugawa vitambulisho vya machinga

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Muktasari:

  • Makonda amewapa wiki moja wakuu wa wilaya za Kinondoni, Ubungo na Kigamboni kuhakikisha wanamaliza mchakato wa ugawaji wa vitambulisho huku akiwapongeza  wakuu wa wilaya za Temeke, Felix Lyaniva na Ilala, Sophia Mjema kwa kukamilisha kwa ufanisi ugawaji wa vitambulisho hivyo.

Dar es Salaam.  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewapa wiki moja wakuu wa wilaya za Kigamboni, Kinondoni na Ubungo kuhakikisha wanakamilisha mchakato wa ugawaji wa vitambulisho.

Katika suala hilo, Makonda amewapongeza wakuu wa wilaya za Ilala, Sophia Mjema na Temeke, Felix Lyaniva kwa kumaliza kwa ufanisi mchakato wa ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo maarufu ‘wamachinga’.

Makonda ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Aprili 2, 2019 wakati akizungumza na wanahabari ofisi kwake, Ilala na amewataka wakuu hao wa wilaya kuchangamka na ndani ya wiki vitambulisho hivyo viishe.

“Nataka wamachinga wote wapate vitambulisho na isitokee watu waendeshe shughuli zao bila vitambulisho. Vitambulisho hivi ni kwa mwaka mmoja tukichelewa kugawa kwa wakati matokeo yake mwakani tutapata shida nyingine.

“Naomba waongeze kasi ya kuwasimamia watendaji wao kila mtaa na kata vitambulisho vimefika. Kabla ya mwisho wa wiki sitaki kusikia habari ya vitambulisho bali ibakie suala la kusimamia sheria,” amesema Makonda.

Kwa mujibu wa Makonda Dar es Salaam, imepatiwa vitambulisho 175,000 huku kila wilaya za Ubungo, Kinondoni, Temeke na Ilala zikipewa  37,000 na Kigamboni 27,000 kulingana na idadi ya watu.