Makonda azindua soko la madini Dar, atoa neno kwa wafanyabiashara

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amezindua soko la kimataifa la madini mkoani humo na kuwataka wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria na kutoshirikiana na matapeli

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amezindua soko la kimataifa la madini mkoani humo na kuwataka wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria na kutoshirikiana na matapeli.

Ametaka soko hilo kuwa chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam na kutoa rai kuwa mtu yeyote atakayeuziwa madini feki maeneo mengine asiwasumbue polisi.

“Soko lipo manunuzi yote yafanyike kwenye hapo na litumike kuwakutanisha wafanyabiashara na wanunuzi wote, mtu akinunua madini mtaani asitusumbue na kuongeza kesi vituo vya polisi,” amesema Makonda leo Jumatano Julai 17, 2019 katika uzinduzi huo.

Amewahakikishia usalama wafanyabiashara wa madini pamoja na wateja,” Soko liwe chombo cha kuwaleta pamoja shirikianeni na muwe sauti moja.”

Mwakilishi wa shirikisho la wachimbaji madini,  Osman Tharia ameshukuru Serikali na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufungua soko hilo.

“Ombi letu kwa wafanyabiashara wa vito wajiunge kwenye chama chetu maana mwitikio umekuwa mdogo,  lengo letu tutambulike popote ili tupate fursa ya kujadili mambo mbalimbali na kusaidiana kwa karibu kuliko hali ilivyo sasa,” amesema.