Malecela, Mbatia watoa neno kifo cha Mengi

Waziri Mkuu mstafu wa Tanzania, John Malecela

Muktasari:

  • Reginald Mengi ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia jana Alhamisi Mei 2, 2019 akiwa Dubai mwili wake unatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu Mei 6 na utazikwa Mei 9, 2019 nyumbani kwake Machame mkoani Kilimanjaro

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstafu wa Tanzania, John Malecela amesema Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi atabaki kwenye mioyo ya watu kutokana na mema aliyoyafanya.

Malecela ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 3, 2019 alipofika kutoa pole nyumbani kwa Mengi Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amesema mtu anapotenda mema baada ya kufa hubaki kwenye mioyo ya watu, hivyo Mengi kutokana na mema aliyoyatenda ataendelea kubaki kwenye mioyo ya watu.

"Yupo mwanafalsafa kutoka Morocco alisema tutakapokuwa tumekufa na tumezikwa kwenye makaburi, msitutafute kwenye makaburi ya chokaa bali kwenye mioyo ya watu," amesema Malecela.

Amesema Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa mema aliyoyafanya, kwani alikuwa mtu wa watu na ataendelea kubaki kwenye mioyo ya watu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR –Mageuzi, Jamesi Mbatia amesema wataendelea kumkumbuka kwa mchango wake katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu.

Mbatia amesema katika kitabu chake cha I can, I Must, I Will kitakuwa msaada mkubwa na kitawasaidia watu kuondokana na umaskini hasa kitakapotafsiriwa.

"Tutamkumbuka mzee Mengi jinsi alivyodumisha mshikamano, ametoa mchango katika sekta nyingi hapa nchini," amesema Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo.

Naye Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Anna Kilango Malecela amesema ataendelea kumkumbuka Mengi kutokana na mchango wake wa visima akiwa Mbunge wa Same.