Malecela asimulia alivyotapeliwa kiwanja Dodoma

Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela ameelezea alivyokumbana na utapeli wa kiwanja chake kilichouzwa mamilioni ya fedha na wahusika kugawana fedha hizo.

Akizungumza jana, Malecela alisema tukio hilo hawezi kulielezea zaidi kwani lipo mikononi mwa vyombo husika, lakini akasema ni la aibu kwa watu wazima na waliopewa dhamana ya wananchi.

Jana, ilikuwa siku ya 14 diwani wa Makole (CCM), Habel Shauri (CCM) kushikiliwa kituo cha polisi kati Dodoma kwa tuhuma hizo huku polisi wakieleza kuwa uchunguzi ukikamilika, atafikishwa mahakamani.

Mbali na Shauri, wengine ni msaidizi wa Malecela, Jackson Ndahani na mwingine aliyetajwa jina moja la Shaaban huku mwanasheria anayedaiwa kupiga mhuri katika hati hiyo hajulikani alipo.

Kwa pamoja wanadaiwa kuuza eneo la Malecela Mtaa wa Area D kata ya Makole kwa Sh35 milioni na mnunuzi alilipa Sh25.5 milioni akibaki na deni la Sh10milioni

Malecela alisema jana kuwa mchezo huo ulianza kimyakimya hadi mnunuzi alipotilia shaka baada ya kukutana na usumbufu katika hati ya kiwanja katika Wizara ya Ardhi.

“Maeneo yote walimaliza kubadili majina isipokuwa Wizara ya Ardhi walikutana na ugumu, hadi Jiji walikuta jina la Ndahani lakini wizarani akakuta Malecela ndipo akaanza kuhofia.”

Msaidizi mwingine wa Malecela, Peter Yobwa alisema katika kufuatilia walikuta taarifa zilizoonyesha uhamishaji wa kiwanja hicho ulifanyika Julai, 2018 lakini mauziano yalifanyika Juni 2018 ikionyesha muuzaji alianza kuuza kabla kupewa hivyo ikatia shaka.

Kamanda wa polisi mkoani Dodoma Gilles Muroto alisema jana kuwa polisi inaendelea kuwashikilia watuhumiwa na akaahidi leo ataitisha mkutano na waandishi kuzungumzia jambo hilo.