Mali za mganga wa kienyeji zachomwa moto akidaiwa kuhusika mauaji ya watoto

Muktasari:

Wananchi wenye hasira wamedaiwa kuchoma moto nyumba na gari vyote mali ya mganga wa kienyeji anayedaiwa kuhusika na mauaji ya watoto wawili  wakazi wa mtaa wa Vuta kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa

 

Sumbawanga. Wananchi wenye hasira wamechoma  moto nyumba na gari vyote mali ya mganga wa kienyeji anayedaiwa kuhusika na mauaji ya watoto wawili wakazi wa mtaa wa Vuta kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Machi 23, 2019 Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Mathias Nyange amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa tayari mganga huyo na mtoto wake  wa kiume wanashikiliwa na polisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Nyage watoto hao wawili ambao miili yao imekutwa katika nyumba ambayo haijamalizika kujengwa jirani na nyumba ya mganga huyo ni Emmanuel Juma (4) na Nicolaus Mwambije (7), mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Kizwite.

Wakizungumza na Mwananchi majirani wa mganga huyo wamesema watoto hao wakiwa na mwenzao mmoja aliyenusurika, walitoweka nyumbani kwao tangu Machi 21, 2019.

Mmoja wa majirani hao kwa sharti la kutotajwa jina amesema mtoto aliyenusurika alionekana leo asubuhi akiwa amejaa matope mwili mzima, taarifa ilitolewa kwa ndugu zake.

“Huyo mtoto alitueleza kuwa wenzake wapo katika gari bovu la mganga huyo na baada ya kuangalia katika gari hilo hatukuwakuta,” amesema.

 

“Tulipokwenda katika nyumba moja ambayo haijamalizika tulikuta miili ya watoto hao ikiwa imetupwa na tukatoa taarifa polisi, mtoto huyo ambaye amenusurika tulimpeleka hospitali, kwa sasa amelazwa.”

Jirani humo amesema mtoto huyo ndio alisaidia kupatikana kwa miili hiyo kwa kuwa walipomhoji aliwaeleza kuwa aliambiwa na mganga huyo aende nyumbani kwa kuwa wenzake wameshafariki dunia.

Alibainisha kuwa baada ya kusikia maelezo ya mtoto huyo majirani walishikwa na hasira na kuvamia nyumba ya nganga huyo na kuchoma moto vitu mbalimbali, ikiwemo gari hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo alifika eneo la tukio na kuwataka wananchi wasijichukulie sheria mkononi na kumuagiza kamanda wa polisi mkoani humo kuchunguza vibali vya waganga wa jadi waliopo Rukwa.