Malima awasha moto akidaiwa kumuweka ndani diwani Chadema kwa kukunja nne

Muktasari:

  • Diwani huyo alisema alikaa ndani kwa saa saba kuanzia saa tisa alasiri hadi saa tatu usiku, “baada ya viongozi wangu wa chama kufanya taratibu za kuniwekea dhamana, lakini nikatakiwa kurudi polisi Jumatatu.

Tarime. Kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima juzi kuamuru kuwekwa mahabusu Diwani wa Kata ya Susuni (Chadema), Abiud Solomon kwa madai ya kuonyesha dharau kwenye kikao chake cha kumtambulisha mkuu mpya wa Wilaya ya Tarime, Charles Kabeho, kimezua mjadala mitandaoni.

Hatua ya mkuu huyo imekuja baada ya Jumanne iliyopita, Rais John Magufuli kuwataka wakuu wa wilaya na mikoa kutafakari kabla ya kuwaweka ndani wananchi kwa makosa mbalimbali.

Alipoulizwa jana kuhusu hatua yake hiyo licha ya kuwapo kwa tamko la Rais, Malima alijibu, “Hilo ni jambo dogo sana,” huku akisema si kweli kwamba diwani huyo alikuwa amekunja nne kama inavyodaiwa kwenye mitandao, bali alikuwa amekaa huku akiwa ameegemea kiti na miguu yake akiwa ameiweka juu ya meza, jambo ambalo alisema ni dharau.

Alidai kuwa alimsimamisha na kumuomba atoke nje kwa vile alionekana hakuwa kwenye kikao hicho, agizo ambalo alisema diwani huyo alitii, “Alipotoka niliendelea na kikao na wala sikuwa na taarifa kama alikamatwa au la, mtafute katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, (Chacha) Heche azungumzie hili,” alisema Malima.

Heche hakupatikana kwani simu zake za mkononi ziliita bila kupokewa. Hata hivyo, mhusika wa tukio hilo, diwani Solomon alipoulizwa alidai kwamba lilitolewa agizo kwa Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe kumweka ndani kwa madai ya kuonyesha dharau kwenye kikao cha mkuu huyo wa mkoa.

“Nilipata nafasi ya kukaa eneo la waandishi wa habari. Sasa ili kuwapisha wapite, nililazimika kubebanisha miguu yangu (kuweka nne) ili kutoa nafasi ya wao kupita na kufanya kazi yao vizuri, kitendo cha mimi kukunja miguu ndiyo mkuu wa mkoa alikichukulia kuwa nimemdharau,” alidai Solomon.

Alisema kabla ya kupelekwa ndani, alihojiwa na mkuu huyo wa mkoa kuhusu wadhifa wake na chama chake, “Kabla sijakaa sawa alitoa agizo la mimi kuchukuliwa na kwenda kuwekwa ndani,” alidai.

Diwani huyo alisema alikaa ndani kwa saa saba kuanzia saa tisa alasiri hadi saa tatu usiku, “baada ya viongozi wangu wa chama kufanya taratibu za kuniwekea dhamana, lakini nikatakiwa kurudi polisi Jumatatu.”

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda Mwaibambe alisema diwani huyo alifanya fujo, “Lakini baadaye aliachiwa, nilikuwapo kwenye kikao.”

Katibu wa Chadema Jimbo la Tarime Vijijini, Sunday Magacha alisema kitendo hicho kilipoteza furaha waliyokuwa nayo ya kumpokea kiongozi wa wilaya maana kimewajengea hofu.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliweka picha ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakiwa wamekunja nne na chini ya picha hiyo ameandika, “Mnafanya kosa kukaa hivi?”

Mwingine aliyeandika katika mtandao wa Twitter akijitambulisha kuwa ni mdude Chadema, alimshauri diwani huyo kutafuta wakili na kufungua kesi mahakamani athibitishe kama kukunja nne ni kosa kisheria.