Mama Mobeto: Bado tupo mjengoni, tutahama Mungu akipenda

Wednesday May 22 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Dar es Salaam. Shufaa Rutiginga, ambaye ni mama mzazi wa mwanamitindo Hamisa Mobeto, ameongelea kuhusu sakata la nyumba inayodaiwa kuwa wameondoka baada ya kushindwa kulipa kodi.

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii picha za nyumba hiyo ya ghorofa moja ziligaa, kuwa madalali wanainadi kwa wapangaji wengine, hali iliyotafsiriwa na baadhi ya wanaofuatilia maisha ya mlimbwende huyo ambaye ni mzazi mwenzie na Diamond Platnumz,  kuwa huenda kashindwa kulipa kodi.

Akizungumza na Mwananchi, Mama Mobeto  alisema hata yeye kaiona nyumba hiyo ikinadiwa mtandaoni  na madalali kama walivyoona watu wengine.

Amefafanua kwamba kwa kuwa wengi wanaijua nyumba ya Hamisa wamedhani ni yake lakini ukweli ni kwamba zinafanana tu kwani wanapoishi kuna nyumba tano za aina hiyo.

“Katika nyumba hizo tano wapangaji wengi wanaokuja kuishi hapa ni wazungu, ambao baadhi yao wanafanya kazi kwa mikataba hapa nchini hivyo wakimaliza huwa wanaondoka, na hivyo mmiliki wa hizo nyumba kuwapa kazi madalali kutafuta wapangaji wengine na ndicho kilichoonekana mtandaoni, lakini ukweli nyumba hiyo sio tunayoishi sisi bado tupo sana na ikifika mahali tukitaka kuhama tutafanya hivyo,” alisema mama Mobeto.

Advertisement