Mama ajifungua watoto wanne kwa mpigo

Thursday January 10 2019

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Jenipher Juma (23), mkazi wa Ibanda jijini Mwanza amejifungua watoto wanne miezi miwili kabla ya siku ya makadirio aliyotarajiwa kujifungua.

 

Jenipher ambaye huo ni uzao wake wa pili alijifungua mchana wa jana Jumatano Januari 9, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza ya Sekou-Toure.

 

Mama huyo amejifungua watoto wawili wa kiume na wawili wa kike ambao hali zao zinaendelea vizuri.

 

Huo ni uzao wake wa pili baada ya ule wa kwanza wa Aprili, 2018 ambapo pia alijifungua watoto wanne kwa wakati mmoja kwa njia ya upasuaji.

 

“Bahati mbaya watoto wangu wa kwanza walifia tumboni miezi mitatu kabla ya muda wa kujifungua ikabidi nifanyiwe operesheni,” alisema Jenipher.

 

Muuguzi kiongozi wa wodi ya wazazi, Tatu Lusesa akizungumza leo Alhamisi amesema safari hii Jenipher amejifungua salama kwa njia ya kawaida na watoto wote wanaendelea kuwa chini ya uangalizi maalumu kutokana na kuzaliwa wakiwa chini ya uzito wa kawaida.

 

“Watoto watatu wamewekwa kwenye kifaa maalumu cha kuwasaidia kuvuta hewa wakati mmoja yuko katika hali ya kawaida na anapumua mwenyewe,” amesema Lusena.

 

Amesema watoto hao wamelazimika kuwekwa chini ya uangalizi maalumu wa kitaalamu kutokana na kuzaliwa kabla ya muda wakiwa na uzito mdogo ambapo mmoja ana kilo moja wakati mwenye uzito mkubwa kuliko wote ana kilo 1.5.


Advertisement