VIDEO: Mama wa pacha 4 afunguka sababu za kupewa talaka

Dar es Salaam. Wakati akiwa katika changamoto za ulezi wa watoto wanne pacha, Radhia Solomon (24) amepata pigo baada ya kupewa talaka na mumewe siku 90 tangu ajifungue watoto hao.

Mwananchi ilibaini hali hiyo jana baada ya kumtembelea binti huyo mtaa wa Idrisa Magomeni kujua maendeleo ya pacha hao.

Radhia aliyejifungua watoto hao Januari 8, alisema hana fedha yoyote ya kujikimu na watoto alioachiwa na mumewe ambaye pia amebeba samani zote.

Hata hivyo, mwanaume huyo Fammy Suleiman (28) alipotakiwa kuelezea sababu za uamuzi wake wa kutoa talaka moja na kuondoka na samani zote za nyumbani, alisema kwa ukali kuwa hataki kuzungumzia mambo ya familia kwenye vyombo vya habari.

“Sitaki mambo ya vyombo vya habari, huyo mpaka mnamtafuta hamjui kama ni mke wa mtu? Haya ni mambo ya familia tutayazungumza kama familia hamhusiki katika hili,” alifoka.

Mama mzazi wa Radhia, Esther Mtinda alisema ameshtushwa: “Kwa kweli imenishtua sana siwezi kuelezea, na hili limetokea nikiwa hapa sina namna siwezi kumtupa mwanangu katika hali hii.”

Mmiliki wa nyumba aliyoishi Fammy na mkewe, Dali Yusuph alisema alipigiwa simu na Fammy akimweleza kuwa amehama.

“Kuna mengi na hapa ananipigia simu akitaka kurejeshewa fedha za pango anasema amehama na miezi miwili iliyobaki Sh260,000, nimemuita kutaka tuyazungumze huyu aliyekuwa mkewe akiwapo sababu watoto ni malaika hawapaswi kufanyiwa haya,” alisema Yusuph.

Mwananchi ilipomtafuta kiongozi wa kidini wa eneo hilo, Ustaadhi Salum Haji alisema wanandoa hao wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara hata kabla ya Radhia hajapata ujauzito wa pacha hao.

“Nimekuwa nikiwasuluhisha mara kwa mara na kuwasihi kila mmoja awe (mwanaume) mvumilivu basi likaenda salama mpaka amepata ujauzito na kujifungua,” alisema.

Ustaadhi Salum aliyekiri kutolewa kwa talaka hiyo, alisema alipigiwa simu na Radhia Aprili 5 akimuomba msaada na alipofika nyumbani kwake, Fammy aliwasili na kumkabidhi mkewe talaka.

“Ninafika pale akampa talaka mbele yangu, nimemshauri mumewe lile ni jukumu lake asilikimbie,” alisema.

Alipotafutwa mwenyekiti wa mtaa wa Idrisa, Issa Sakatara alisema Ijumaa alipigiwa simu na Radhia akimfahamisha ana shida baada ya kufika alimweleza kuhusu talaka hiyo.

“Alikuwa amechanganyikiwa nikamsihi atulie, awe mvumilivu, Jumatatu (leo) niweze kulifanyia taratibu za kiofisi,” alisema.