Mama waziri alivyoanza mamalishe kwa kukopa mchele

Muktasari:

  • Mbali na mchele, alikopa tenga la kuku 30 na nyama ya ng’ombe alikuwa akipelekewa kutoka ranchi ya Mkwaja kwa Sh400 kwa kilo.

Tanga. Wapo watu hujiuliza maswali jinsi ya kupata mtaji wa biashara, lakini usikubali mawazo yatatize ndoto yako kwani unaweza kupata mtaji kwa akili ndogo.

Fatma Omari Masanga (55), mama wa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema alianza shughuli ya mamalishe kwa kukopa mchele, lakini sasa biashara hiyo imempa manufaa makubwa.

Mkazi huyo wa Bweni, Pangani mkoani Tanga katika mahojiano na Mwananchi yaliyoanza kuchapishwa jana, alisema alianza biashara hiyo katika kijiji cha Sakura kwa kukopa gunia la mchele la kilo 80 katika duka la mfanyabiashara mmoja.

Mbali na mchele, alikopa tenga la kuku 30 na nyama ya ng’ombe alikuwa akipelekewa kutoka ranchi ya Mkwaja kwa Sh400 kwa kilo.

“Nilianza kwa kuuza wali kuku kwa Sh200, chai Sh10 na andazi Sh5. Chapati niliuza kwa Sh5, supu ya kuku Sh100 na supu ya samaki Sh100,” anasema mama huyo akizungumzia bei za zamani alipoanza biashara hiyo.

Anasema sasa sahani moja ya wali nyama anauza kwa kati ya Sh1,000 hadi 1,500.

“Kikombe cha chai Sh200, supu ya kuku na samaki Sh2,000, chapati Sh200 na andazi Sh100. Pilau nauza Sh1,000 hadi Sh 1,500.”

Kuhusu mtaji na faida anayopata kwa siku, Fatma anasema hiyo ni siri yake.

“Katika biashara kuna siri, siwezi kubainisha hasa kama mauzo yangu kwa siku ni kiasi gani kwa sababu kuna wakati nikiwa safarini huwaachia wadogo zake Jumaa kuendesha biashara hii. Kwa hiyo nikirejea ni rahisi kuwabana nikikuta hesabu hazijaenda ipasavyo,” anasema.