Mamba waua watu wanne Sengerema

Buchosa. Mamba na fisi wamekuwa tishio kwa watu wanaozunguka Ziwa Victoria katika Halmashauri ya Buchosa, Sengerema mkoani Mwanza.

Katika mwezi huu pekee, watu wanne wameliwa na mamba hivyo kufanya idadi ya walioliwa kufikia 13 huku wengine watano wakijeruhiwa tangu mwaka 2016. Fisi wameua watu wawili na kujeruhi wengine wawili.

Kaimu ofisa ardhi na maliasili Halmashauri ya Buchosa, Aliko Ndile alisema jana kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kunusuru maisha ya watu.

Ndile aliyataja maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na wanyama hao kuwa ni vijiji vya Kanyaku, Kisaba, Nyambeba na Izindabo cha Kata ya Buhama kisiwani Kome Mchangani.

“Kweli hali hii inatishia uhai wa binadamu, maana watu 16 sio mchezo kuliwa na wanyama hao,” alisema Ndile.

Mwenyekiti wa makambi ya Kome Mchangani, Ntabaguzi Angelo alisema mwezi huu umekuwa wa majonzi katika eneo hilo baada ya watu wanne kupoteza maisha kwa kuliwa na mamba wakiwa wanaoga ndani ya Ziwa Victoria.

Amiri Soko ambaye alimpoteza mtoto wake aitwaye Hussen (24) alisema mwanaye alimuaga anakwenda kuoga na wenzake katika mwalo wa Chilogo saa 10 jioni lakini hakurejea na watu walionusurika ndio waliotoa taarifa za kuchukuliwa na mnyama huyo.

Mmoja wa watu walionusurika kuliwa na mamba katika eneo hilo, Amina Salumu alisema wamezoea kuoga ziwani ndio maana inakuwa rahisi kuliwa na wanyama hao.

Katika kukabiliana na tishio la mamba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda alisema wamechimba visima 14 kwenye maeneo ambayo watu wanaliwa na kujeruhiwa na wanyama hao ili wasiende ziwani.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema ili kukabiliana na janga hilo, ipo haja ya kuweka sheria ndogondogo ya zuio la watu kuoga ziwani.