Mambo 14 yatakayoimarisha mapato Zanzibar 2019/20 yabainishwa

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka 2019/20 huku akibainisha mambo 14 yatakayowezesha kuimarisha mapato ya kipindi hicho.


Unguja. Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa ametaja mambo 14 kuwa ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha mapato ya Serikali ya Zanzibar katika kipindi cha mwaka 2019/20.

Balozi Ramia ameyataja mambo hayo leo Alhamisi Juni 20, 2019 katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20.

Ameyataja mambo hayo ni kuifanyia marekebisho sheria ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kutoa kodi kwa wageni wanaolala kwenye vyombo vya baharini, kujumuisha gari za mizigo zenye uwezo wa kubeba chini ya tani moja na nusu katika utaratibu wa ushuru wa stemp, kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato katika wizara na taasisi za Serikali.

Mengine ni kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mapato, kugomboa madeni ya walipa kodi, kuongeza muda na ufanisi wa utoaji na usafirishaji mizigo kupitia bandarini, kuwatangaza walipa kodi wanaokwepa kulipa kodi, kuwajengea uwezo watumiaji wa mfumo wa Forodha (TANCIS), kupambana na njia zinazotumika kuepuka kodi (Tax Avoidence).

Waziri huyo ameyataja mengine kuwa ni kuwaelimisha wananchi kudai risiti za kielektroniki, kuifanyia mapitio sheria na kanuni zinazotoa misamaha ya kodi, kufuatilia miongozo ya kimataifa ya misamaha ya kodi kwa miradi ya maendeleo, kuondoa zuio (Rentetentio) la mapato kwa taasisi za Serikali.