Mambo matano niliyoyaona Wasafi Festival

Muktasari:

Mchanganyiko wa wasanii wa zamani na sasa, Bongo Movie na Bongo Fleva ulipendezesha tamasha hilo ambalo litafanyika katika mikoa mingine minne Tanzania

Mwishoni mwa wiki iliyopita tamasha la Wasafi liling’oa nanga likianzia mkoani Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda.

Miongoni mwa mambo mazuri niliyoyaona ni pamoja na wasanii wengi kushirikishwa hali ambayo ilisaidia kukata kiu ya mashabiki wa burudani.

Mchanganyiko wa wasanii wa zamani na sasa, Bongo Movie na Bongo Fleva ulipendezesha tamasha hilo ambalo litafanyika katika mikoa mingine minne nchini.

Uwepo wa wasanii kama Dudu Baya, Nikki Mbishi, One Incredible, Chin Beez, Moni Centrizone na wengineo kutoka lebo ya Wasafi uling’arisha usiku huo.

Waigizaji Steve Nyerere, Aunty Ezekiel, Welo Sengo na Jackline Wolper walikamilisha safu kwa kuwa wawakilishi wa Bongo Movie.

Ushiriki wa Serikali katika shughuli nzima ulionyesha kwa kiasi gani Wasafi kama kampuni inaheshimu mamlaka na pia inapunguza uwezekano wa uwepo wa janja janja katika uandaaji wa tamasha hilo.

Serikali inaposhirikiana na watu wake inaongeza imani kwa wananchi kwamba lina nia njema katika kukuza muziki na kuwainua wasanii. Kabla ya kuhitimisha kwa burudani, wasanii walioshiriki walitoa misaada kwa wajane na wasiojiweza. Wasanii hao wakiongozwa na Diamond Platnumz walitoa misaada mbalimbali kwa wenye uhitaji.

Mchanganyiko wa Diamond na wasanii wengine ulikuwa wa kuvutia, tofauti na ilivyotarajiwa kuwa kwa kuwa Diamond ndiye mmiliki wa tamasha na msanii mkubwa alitarajiwa kuwa tofauti.

Wakati wote alionekana kujiweka karibu na wenzake na hata wakati wa kutumbuiza hakujionyesha wa tofauti. Wasanii wote walionekana wenye furaha na huru kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

Jambo la kuboresha katika tamasha hilo katika siku za usoni ni ushiriki wa wasanii chipukizi kuwa wengi na hivyo kuchelewesha wasanii wakubwa kupanda jukwaani.

Ni sahihi kuwashirikisha wasanii wanaotafuta njia ya kutoka lakini si vyema kuwa nao wengi kwani hilo lilisababisha tamasha rasmi kuchelewa kuanza.